SERIKALI inatarajia kuwalipa fidia ya sh bilioni 70 wakazi wa eneo la Kurasini watakaobomolewa nyumba zao ili kupisha upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam.
Mpango wa upanuzi wa bandari ulibuniwa na serikali tangu mwaka 1994.
Meneja Mradi wa Kuendeleza Upya Eneo la Kurasini kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Mhando, alisema jana katika mkutano wa hadhara kuwa, wakazi 34,432 waliopo katika kaya 2,426, watakumbwa na hamisha hamisha.
Alisema mpango huo umeandaliwa kukidhi ongezeko la mahitaji ya bandari, kama maghala, hifadhi ya mafuta na miundombinu, na kutokana na kuwa na ongezeko kubwa la mizigo kutoka ndani na nje ya nchi ambayo inahitaji nafasi.
“Lengo la mradi ni kupata ardhi kwa ajili ya huduma za bandari, kuboresha mazingira na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa bandari ya Dar es Salaam, ni hazina kubwa ya uchumi wa nchi hivyo ni muhimu kuiwezesha kutoa mchango mkubwa katika ukuaji uchumi na kupunguza umasikini,” alisema Mhando.
Lengo jingine, alisema ni kuongeza ufanisi na utendaji wa bandari, kupunguza msongamano wa mizigo na kuongeza uwezo wa kuhifadhi mizigo katika eneo la bandari, kuongeza ufanisi na utendaji wa bandari, kukabiliana na ushindani wa bandari za Kenya, Msumbiji na Afrika Kusini, na kuimarisha usalama.
Jingine ni kuongezeka kwa uwekezaji katika kilimo, viwanda, madini, usafirishaji, utalii na uhusiano wa kimataifa, kuongeza pato la taifa, kupata ajira katika miradi itakayoanzishwa, kuwezesha wananchi kuondokana na makazi holela.
Aliitaja mitaa ya eneo la Kurasini itakayokumbwa na hamisha hamisha hiyo kuwa ni Kurasini, Mivinjeni, Minazini, Shimo la Udongo na Kiungani.
Alisema pia wakazi wa Mtaa wa Sabasaba katika Kata ya Mtoni, wataathiriwa kwa kiasi fulani. Kwa kuanzia mradi huo utaanza eneo la Shimo la Udongo.
Alisema eneo la mabwawa ya maji machafu katika Mtaa wa Shimo la Udongo litaathiriwa na mpango huo na kuwa maeneo yenye mahitaji muhimu kama makanisa, shule, misikiti na masoko hayataathiriwa.
Alisema mpango huo umeandaliwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji na wadau wengine. Unatarajiwa kukamilika mwaka 2012.
“Mpango huu utatekelezwa kwa awamu hadi mwaka 2012, utekelezwaji wake utakuwa endelevu kwa kuzingatia urejeshwaji wa gharama, ni mojawapo ya mikakati ya Wizara ya Ardhi ya kutekeleza sera ya serikali ya kuboresha makazi mijini,” alisema Mhando.
Kwa mujibu wa Mhando, uthamini wa ardhi na nyumba utaanza baadaye mwezi huu hadi Agosti, mwaka huu, ulipaji wa fidia utakuwa kati ya Agosti na Septemba, upimaji wa viwanja ni Oktoba na ugawaji wa viwanja na utoaji wa hati utakuwa kati ya Novemba na Desemba, mwaka huu.
Naye, mthamini wa mradi huo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Yahya Mbalilaki, alisema fidia zitalipwa kwa kuzingatia haki.
Alisema thamani ya nyumba itajulikana kwa jinsi itakavyokuwa. Ekari moja italipwa sh milioni 20, na mazao ya kudumu yatalipwa fidia.
Pamoja na ulipwaji wa fidia za nyumba bila kujali kuwa ni robo ekari, mwenye nyumba atalipwa fedha za miaka mitatu kwa jengo (nyumba) atakalohama, atalipwa kwa muda wa miaka mitatu kama usumbufu wa kumhamisha.
Alisema kazi nzima itasimamiwa kwa umakini na viongozi mbalimbali, wakiwamo wenyekiti wa Serikali za Mitaa ili kutoruhusu utapeli na dhuluma.
Meneja Mradi wa Viwanja 20,000 Mkoa wa Dar es Salaam, Venant Mugemuzi, aliwataka waliokuwa na migogoro ya viwanja, wakiwamo wanawake waliojenga nyumba hizo na waume zao na baadaye kuachana, waandae vielelezo mapema ili waweze kusaidiwa.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Zablon Masele, alisema wananchi watakaoathiriwa na mpango huo watahamia eneo la Kibada.
“Rasilimali ya msingi kwa binadamu ni ardhi, hivyo lazima tupange jinsi ya kuitumia kulingana na mahitaji ambayo yanabadilika kila siku, faida ya kufanya hivyo ni kubwa,” alisema Masele.
Mkuu wa Wilaya (DC) ya Temeke, Baraka Konisaga, aliwaahidi wananchi kusimamia kazi hiyo kwa makini.
Awali, Diwani wa Kata ya Kurasini, Wilfred Kimati, aliiomba serikali kuhakikisha wananchi wanapewa eneo zuri kwa ajili ya makazi yao mapya.
Aliwaondoa wasiwasi wananchi na kuwataka wawe watulivu.
Pamoja na Konisaga, wengine waliohudhuria mkutano huo ni viongozi mbalimbali wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Manispaa ya Temeke, akiwamo Meya Jerome Bwanausi, na viongozi wengine wa Kata ya Kurasini