MAKAMU wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, yuko London, Uingereza akipatiwa matibabu ya figo na kufanyiwa uchunguzi wa kawaida wa afya yake.
Taarifa iliyotolewa na ofisi yake jijini Dar es Salaam jana, ilisema Dk. Shein anatibiwa katika Hospitali ya London.
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais, Penzi Nyamunguni, alisema pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa kawaida wa afya yake, Dk. Shein pia atapewa matibabu ili kuondoa vijiwe katika figo zake.
Alisema Oktoba, 2004, wakati akifanyiwa uchunguzi wa afya yake, alibainika kuwa na vijiwe hivyo.
“Kwa wakati huo, ilishauriwa kwamba hakukuwa na haraka ya kufanya matibabu hayo, wataalamu walishauri kuwa yanaweza kufanyika kwa siku za baadaye.
“Sasa imeonekana ni wakati mzuri akafanyiwa matibabu ili kuondoa vijiwe hivyo,” alisema Penzi.
Dk. Shein alifika London akitoka Brazil ambako alimwakilisha Rais Jakaya Kikwete katika mkutano wa kimataifa.
Penzi alisema: “Hali ya Mheshimiwa Makamu wa Rais inaendelea vizuri, anatarajia kurejea nyumbani wakati wowote.”