Na Omari Shaaban, Arusha
KAMPUNI, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na watu binafsi wametakiwa kuchangia maendeleo ya shule kwa kukarabati miundombinu, majengo na kusaidia upatikana wa nyenzo za kufundishia na kujifunzia.
Hayo yalielezwa juzi na Mkuu wa mkoa wa Arusha, Abbas Kandoro wakati akizindua jengo la maabara pamoja na kukabidhi vifaa vyake ambavyo vimetolewa na benki ya CRDB kwa shule ya sekondari ya Sinoni iliyoko mjini hapa.
Kandoro alisema uamuzi wa benki hiyo kugawa sehemu ya faida itokanayo na biashara yake kwa kutoa msaada katika sekta ya elimu una maana kubwa kwa asasi za kibiashara kuwa zinaweza kufanikiwa tu endapo jamii inayozizunguka itakuwa imejikwamua kiuchumi.
"Elimu ni moja ya nyenzo ya kuikwamua jamii kutoka katika umasikini kwani elimu ni urithi bora kwa mtoto ambao kamwe hawezi kunyang'anywa kwa njia yoyote lakini ni silaha kubwa inayompa uwezo wa kupambana na mazingira,'' alisema Kandoro.
Naye mwakilishi wa Mkurugenzi wa benki ya CRDB, Tully Msirikale. alisema wameamua kutoa msaada huo wenye thamani ya sh. milioni tano kwa shule ya sekondari Sinoni kwa kutambua kuwa mafanikio iliyoyapata yametokana na mshikamano uliojengeka kati ya benki na jamii
Msirikale alieleza kuwa katika kutimiza azma hiyo ya kurudisha sehemu ya mafanikio, benki kwa miaka kumi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, imetenga sehemu ya faida iliyotokana na biashara zake na kuchangia maendeleo ya jamii hasa kwenye sekta ya elimu.
Alisema kuwa wamechagua shule mbalimbali kwenye mikoa ambayo benki hiyo ina matawi kwa lengo la kutoa vitabu vya kiada,fedha za kuboresha madarasa,visima vya maji pamoja na vifaa vya michezo
Katika hafla hiyo ya kutoa misaada ya vifaa vya maabara na kuzindua jengo pia Benki ya CRDB ilizindua kampeni ya upandaji miti 2000 katika eneo la shule ya sekondari ya Sinoni pamoja na maeneo ya jirani .