BALOZI wa Tanzania nchini Ujerumani, Bw. Ali Abeid Karume, amesema hana mpango wowote wa kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2010.
Taarifa yake ya faksi kwa gazeti hili jana, ilisema maelezo yaliyotolewa na gazeti hili Julai mosi mwaka huu kuhusu kufikiria kugombea tena baada ya kuchujwa mwaka jana na CCM, hayakuwa na ukweli.
"Sijawahi kusema au kutamka kwa mwandishi wenu au yeyote wa habari, kwamba nafikiria kugombea urais tena...maelezo hayo ya uongo na uzushi yanaweza kuleta mtafaruku baina yangu na Rais wa Tanzania na kuhatarisha ajira yangu serikalini," alilalamika Bw. Karume.
Bw. Karume ambaye anakiri habari hizo pia kuandikwa na gazeti la Mtanzania amesisitiza kuwa hajafikiria bado kuwania kiti hicho cha juu nchini.
Balozi Karume mwaka jana alikuwa mmoja wa wanachama 11 wa CCM waliojitokeza kuwania kugombea urais, lakini hatimaye chama hicho kikawachuja na kubakia Bw. Jakaya Kikwete, ambaye hatimaye aliibuka mshindi na kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne.
Source: Majira