KUNDI la watu wanaojitambulishwa kuwa ni maofisa kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, limeibuka wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Wanadaiwa kuwadanganya wananchi kuwa, wametumwa kuandikisha upya majina ili wananchi hao wapatiwe viwanja vipya.
Matapeli hao, kwa zaidi ya wiki moja sasa wamekuwa wakiendesha operesheni hiyo katika vijiji kadhaa, wakidai walipwe sh 20,000 kutoka kwa kila mwananchi anayemiliki kiwanja.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi katika eneo la tukio, Katibu wa Kitongoji cha Kiharaka, Kijiji cha Mapinga, Joseph Malula, alisema kuwa matapeli hao wamekuwa wakitumia nyaraka mbalimbali ambazo hazikusainiwa na mamlaka husika.
“Hawa watu kwa kweli tunawashangaa, kwani wamekuwa wakifika hapa kijijini huku wakiwa na nyaraka ambazo wanadai zimetoka wizarani, wanatulazimisha kuzijaza na kusaini kwa madai kuwa tutapewa viwanja vingine,” alisema Malula.
Alisema suala hilo limesababisha matatizo makubwa katika kijiji hicho kwani, hatma ya wakazi hao haijulikani kama watanyang’anywa viwanja hivyo ama la.
Aliiomba serikali ichukue hatua za haraka kuwadhibiti watu hao ili kuepusha matatizo yatakayoweza kujitokeza.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bagomoyo, Hawa Ngulume alisema hajapokea taarifa za kuwapo kwa matapeli hao.
Alisema anachofahamu ni kwamba, eneo hilo limevamiwa na wananchi kinyume cha sheria.
Alisema serikali wilayani humo tayari imewaamuru wavamizi wa viwanja katika kijiji hicho waondoke haraka kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.
Alisema kuna zaidi ya wananchi 200 kutoka Boko, Tegeta na Bunju waliovamia viwanja vya watu mbalimbali, kikiwamo cha familia ya marehemu Paul Bomani.
“Hawa ni wavamizi, lazima waondoke tu, wamevamia kiwanja cha marehemu Bomani na Mwaikambo, wewe huoni kwamba wamevunja sheria na kanuni zilizopo? Ofisi yangu haijatoa kibali jamani,” alisema Ngulume.