WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Masoko, Nazir Karamagi, ametalikiana na mkewe, Mzungu mwenye asili ya Urusi.
Habari zilizopatikana Dar es Salaam zilisema, mke huyo amefungua kesi katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, akitaka atendewe haki katika mgawo wa mali.
Pamoja na mgawo, pia anataka apate malipo manono ya fedha kila mwezi ili aweze kumudu hali ya maisha inayomkabili sasa.
Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Catherine Revocat wa mahakama hiyo.
Mawakili kadhaa wamejitokeza kumtetea mama huyo, lakini kwa bahati mbaya, wamekuwa wakijitoa kwa sababu mbalimbali.
Miongoni mwa sababu zilizoelezwa na vyanzo vya habari ni kwamba, wanahofu kutoa dosari uhusiano wao na mmoja wa watu muhimu serikalini, yaani Waziri Karamagi.
Habari zilizopatikana mwishoni mwa wiki zilisema, wakili mwingine aliyekuwa akimtetea mwanamama huyo, naye kajitoa.
Mke huyo anayetambuliwa kwa jina la Nadya Karamagi, sasa ni Mtanzania baada ya kuukana uraia wake wa asili.
Chanzo cha habari kilisema, Nadya anataka alipwe kiasi cha sh 800,000 kwa mwezi tangu alipotelekezwa na Karamagi miaka miwili iliyopita. Pia ametaka nyumba na gari.
Kimsingi, Karamagi amekubali kutekeleza madai hayo, lakini tofauti zilizojitokeza ni kwenye madai ya mke huyo kutaka apewe kianzio kinono cha maisha. Karamagi hataki hilo, na linaelezwa kwamba ndicho chanzo cha suala hilo kufikishwa mahakamani.
Mke huyo sasa anafanya kazi katika Casino ya Las Vegas iliyopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam.
Tanzania Daima haikufanikiwa kumpata Waziri Karamagi, kwa kuwa yuko Nigeria pamoja na Rais Jakaya Kikwete.