Vibanda vinavyoonyesha picha za video vyabomolewa
Na Stan Likomawagi, Morogoro
HALMASHAURI ya manispaa ya Morogoro imeanza kubomoa vibanda vinavyoonyesha picha za video kwa kutoza watu fedha katika maeneo mbalimbali nyakati za usiku.
Mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa hiyo, Rafael Ndunguru, alisema shughuli hiyo imeanza katika maeneo mbalimbali kutokana na vibanda vingi kuonyesha picha za ngono hasa nyakati za usiku.
Alisema wapo watu wengi wanaonyesha picha za ngono kwenye vibanda vyao kwa kuwatoza watu sh. 50 kwa mtoto na watu wazima sh. 100.
Aliongeza kuwa hali hiyo ni hatari kwa kuwa hata watoto wadogo wanaingia katika vibanda hivyo na kujifunza vitendo vinavyochochea maambukizi ya ukimwi.
Ndunguru alisema mpaka sasa tayari amemkamata mkazi wa Chamwino na kumfikisha kituo cha polisi. Alidai mtu huyo ambaye amejenga kabisa banda lake amekuwa na tabia ya muda mrefu ya kuonyesha picha za ngono.
"Yule kijana nilimkamata juzi lakini wakati nampeleka polisi akaruka kwenye gari leo (jana) tumefanikiwa kumkamata na naagiza wakazi wa Morogoro waache kabisa tabia hiyo,"alisema Ndunguru.
Mkurugenzi huyo alisema tayari amevunja zaidi ya vibanda vitano vilivyopo katika mitaa ya Mji mpya, Chamwino, Kichangani na Misongeni.
Aliwataka wakazi wa Morogoro kuhakikisha wanawazuia watoto wao kuangalia picha hizo kwa kuwa zinawafundisha maadili yasiyofaa.