Na Peter Orwa
TANZANIA itatoa msaada wa pikipiki 50 kwa ajili ya uchaguzi mkuu Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Asha–Rose Migiro aliwaambia wa habari ofisini kwake jana kuwa, msaada huo utatolewa kupitia kikao cha Jumuia ya Mabunge ya Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Alikuwa akieleza yaliyojiri katika kikao hicho cha SADC kilichofanyika Kinshasa, DRC kwa siku mbili Julai 14 na 15.
Tanzania pia imeahidi kutoa waangalizi wa uchaguzi, baadhi yao wakiwa ni maofisa wa wizara yake na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano.
Alisema SADC kwa ujumla, imeahidi kutoa waangalizi 200 wa kijeshi na kiraia watakaoripoti mwenendo wa uchaguzi kuutathmini kama ni wa huru na haki.
Waziri Asha Migiro alifuatana na Waziri wa Ulinzi, Profesa Juma Kapuya, ambao walihudhuria mkutano wa Mabunge ya SADC ya Ulinzi, Siasa na Usalama, walirejea juzi usiku. Tanzania ni Makamu Mwenyekiti ambapo Mwenyekiti wa sasa ni Namibia.
Alisema nchi nyingine zimechangia baadhi ya vifaa kama ndege na helikopta na kurahisisha usambazaji wa karatasi za kupigia kura katika uchaguzi huo utakaofanyika Julai 30, mwaka huu.
Kuhusiana na maandalizi, Dk Asha, alisema tathmini ya SADC imeridhika nayo, licha ya kuwepo matukio kadhaa ya uvunjaji wa amani.
Aliongeza kuwa wajumbe wa SADC wameshuhudia wagombea wakijinadi bila ya kubughudhiwa katika kampeni zao.
Kuna jumla ya wagombea 33 wa nafasi ya urais, akiwemo Rais wa sasa Joseph Kabila na wengine 9,000 wanaowania nafasi 500 za ubunge.
Naye Balozi wa DRC nchini, Dk Juma-Alfan Mpango, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wagombea wa nafasi za Urais walilipia dola za Marekani 50,000 (sawa na sh. milioni 60)
Alisema uchaguzi huo unafanyika, baada ya kutofanyika kwa miaka 40, lakini hautawahusisha raia walio nje ya nchi. DRC ina watu milioni 60.