Na Antar Sangali, Mtwara
WAZEE wa Chama Cha Mapinduzi, Mtwara wameiomba Idara ya Itikadi na Uenezi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kufufua vyuo vya siasa na itikadi ili kuwajengea uwezo, umadhubuti na upeo makada wa CCM Bara na Visiwani.
Hayo yalisemwa na wazee hao walipokutana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM wa Itikadi na Uenezi, Aggrey Mwanri, ambaye yuko ziarani mkoani hapa.
Aliyetoa hoja hiyo alikuwa Salum Jaha ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa TANU mkoani Mtwara toka mwaka 1963 hadi 1968.
Jaha akizungumza kwa niaba ya Wazee wenzake mkoani hapa alisema bila ya makada kupelekwa katika vyuo vya siasa kupikwa, kasi ya kujenga Chama ndani na nje ya umma inaweza kulegalega.
Alisema pamoja na kuwajengea mbinu na maarifa zaidi makada wa Chama alishauri kuwa ni vyema wazee wenye uzoefu watakaoshirikishwa katika kukisaidia Chama inapobidi ili kukiimarisha.
Jaha alisema makada wa Chama ni muhimili, nyenzo na vioo vitakavyotoa picha kamili ya kimaadili, kinidhamu na kuonyesha Chama kuwa na rasilimali wanasiasa wake katika kuendeleza uhai wake.
Wakati huo huo, Mwanri alisema mwanachama ama kiongozi atakayeendeleza dhana ya makundi CCM itamtazama kwa jicho la dharau bila ya kumpa uzito wa heshima stahili.
Mwanri alitoa kauli hiyo alipozungumza katika kikao chake na Wazee wa CCM katika Manispaa ya Mtwara Mikindani juzi usiku.
Alisema CCM kamwe hakina makundi wala mitandao baada ya mchakato wa uchaguzi ndani ya Chama kumalizika na kwamba, hivi sasa kina mtandao mmoja tu unaoitwa CCM moja chini ya umoja na mshikimano.
Mwanri alisema CCM kina majukumu makubwa ya kupambana na umasikini wa wananchi, kukuza uchumi na kudumisha umoja wake wa Taifa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ameridhishwa na utamaduni uliopo mkoani Mtwara wa maelewano kati ya wanachama, viongozi wa CCM, Jumuiya zake ikiwa pamoja na ushirikishwaji kikamilifu wa waasisi toka enzi za TANU, ASP na sasa CCM.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mtwara, Mohammed Ndaile, akizungumza kwenye Kikao hicho, ameipongeza Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kwa kumteua Mwanri kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu wa Itikadi na Uenezi baada ya jina lake kupendekezwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.
Alisema ili CCM izidi kukabiliana na ushindani na iweze kushinda kidemokrasia inahitaji viongozi wakongwe katika siasa wanayotumia hazina ya busara na hekima katika kubuni mikakati na wasio na woga wa kutetea sera za Chama, itikadi ya siasa ya Ujamaa na kuilezea katika utaalamu wenye upeo.