Ni kwa kufunguliwa ofisi ya ubalozi Brazil
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Cyril Chami, amesema Tanzania inatarajia kufaidika na uwezo mkubwa wa teknolojia katika uzalishaji, baada ya kufunguliwa kwa ubalozi nchini humo.
Dk. Chami alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J. K Nyerere, Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwasili akitokea Brazil, kuhudhuria mkutano wa wanataaluma wa Afrika na Ughaibuni. Alitoa tafsiri ya Ughaibuni kuwa ni nchi ambazo zina watu wenye asili ya Afrika.
Alisema Brazil na Amerika Kusini kwa ujumla ina hali ya hewa na mazingira yanayofanana na Afrika, lakini Brazil imepiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kama vile miwa na mihogo.
Dk. Chami alitoa mfano wa mihogo, ambayo huzalishwa huko kwa mbegu mbalimbali na kila mbegu ina bodi yake ya masoko, hali inayowapatia wakulima faida kubwa.
Alisema mabaki ya miwa yapatikanayo nchini humo hutumika kutengeneza nishati ambayo ni mbadala wa mafuta ya petroli katika kuendeshea magari na kuwa maeneo kama hayo, Tanzania inaweza kufaidika kwa kujifunza.
Naibu Waziri alisema kufunguliwa kwa ubalozi Tanzania nchini Brazil, kutawezesha kufungua milango ya kiuchumi kwa upana katika bara la Amerika ya Kusini, ambalo hadi sasa inawakilishwa na ubalozi wa Marekani.
Akifafanua, Mkurugenzi wa Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Pastor Ngaiza ambaye alikuwemo katika ziara hiyo, alisema wazo hilo si jipya, kwani limedumu kwa miaka miwili sasa lakini utekelezaji wake ulikwamishwa na ufinyu wa bajeti.
Kwa mujibu wa Balozi Ngaiza, mapendekezo hayo ya kufungua ubalozi yamo katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na iwapo yatapitishwa, utafunguliwa mwakani.
Dk. Chami alizungumza na waandishi wa habari akimwakilisha Makamu wa Rais Dk. Ali Mohammed Sheni, ambaye ameendelea na safari Uingereza.
Alisema Dk. Sheni alifanya mazungumzo na Rais wa Brazil Luiz Ignasio da Silva ‘Lula’ aliyeshauri kwamba Tanzania ifungue ubalozi wake, kama nchi hiyo ilivyofanya kwa kufungua ubalozi wake nchini Tanzania.
Wakati huo huo, mkutano huo wa wasomi wa Afrika na Ughaibuni, umeazimia kuunda tume maalum ya kutekeleza mawazo ya mkutano ulioazimia Afrika kuamka kwa kuwekeza zaidi katika elimu na wasomi wake kurudi nyumbani kuendeleza.
Hata hivyo, mkutano huo uliofanyika katika ya Julai 12 na 14, bado haujainisha jinsi suala hilo litakavyotekelezwa.
Mkutano kama huo ni wa pili kufanyika, ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2004 nchini Senegal.