Na Ester Bulaya
VIONGOZI wa wanne wa kiwanda cha kutengeneza nguo cha Nida Textile Mills ambao ni raia wa Pakistan wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumjeruhi Mtanzania na kumfungia ndani ya kontena.
Waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni Habibu Khan (30) ambaye ni ofisa mauzo, Mohamed Rashid (25), Shazad Hassan Khan (36) ambaye ni mwendesha mashine na Inamu Shamrey Khan (25) mlipa fedha mkuu. Wote ni raia wa Pakistan na wakazi wa Tabata, Dar es Salaam.
Mshitakiwa wa tano Mohamed Khatf (30) ambaye pia ni raia wa Pakistan na mwendesha mashine katika kiwanda hicho hakufikishwa mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa na amelazwa kwenye hospitali ambayo upande wa mashitaka hawana uhakika na hawajui jina la hospitali aliyolazwa.
Kuhusu mtuhumiwa huyo, upande wa mashitaka uliiomba mahakama muda wa kufuatilia ili waweze kupata taarifa rasmi na kama mshitakiwa amelazwa mahakama iende kumsomea shitaka lake hapo alipolazwa.
Akiwasomea mashitaka yao, mwendesha mashitaka Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Charles Kenyela mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Eddy Lyamuya alidai kwamba washitakiwa hao wanatuhumiwa kwa makosa ya kujeruhi na kumfungia visivyo halali ndani kontena.Katika shitaka la kwanza, Kenyela alidai kuwa washitakiwa wote kwa pamoja Julai 12, mwaka huu, saa tano usiku kwenye kiwanda hicho walimpiga kwa nondo na kumjeruhi Kheri Adinani (26) kiunoni, kwenye jicho la kushoto na mguu wa kulia na kumsababishia maumivu makali.
Shitaka la pili watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa baadaye walimfungia Adinani ndani ya kontena kuanzia saa 10 alfajiri hadi saa 12 alfajiri isivyo halali. Adinani anayedaiwa kuwa mfanyakazi wa kiwanda hicho ni mkazi wa Mtoni Kijichi.
Upande wa mashitaka uliiomba mahakama leo uwasilishe hati ya kupinga dhamana dhidi ya washitakiwa kwa sababu mshitakiwa mmoja hakuwepo mahakamani na hawana uhakika wa maelezo kwamba amelazwa hospitali.
Sababu ya pili ya kupinga dhamana iliyotolewa na upande wa mashitaka ni kwamba mlalamikaji katika kesi hiyo Adinani amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hivyo ni muhimu kufuatilia hali yake.
Kenyela akisaidiwa na mwendesha mashitaka Mrakibu wa polisi Willy Mlulu walidai kwamba hati za kusafiria za watuhumiwa hazionyeshi vibali vyao vya kuishi nchini vinaisha lini na hivyo wanaofu wakipewa dhamana wanaweza kutoroka kwa siyo raia wa nchi hii.
Akijibu hoja hiyo wakili wa upande wa utetezi Justunian Byabato alidai kuwa dhamana ni haki ya kila mshitakiwa hata kama akiwa siyo raia mradi shitaka analoshitakiwa linastahili apewe dhamana, kwani wateja wake hawashitakiwi kwa kosa la wizi wa silaha ambalo haliruhusu mshitakiwa kupata dhamana.
Kesi hiyo itaendelea leo. Kesi hiyo ilikuwa na mkalimani kwa upande wa washitakiwa ambaye alikuwa akiwatafsiria watuhumiwa kwa lugha ya Ureu ya Pakistan. Mkalimani alijulikana kwa jina la Abdurhman Malik (38).