MTU anayesadikiwa kuwa jambazi ameingia katika Kituo Kidogo cha Polisi eneo la Mwembe Mchomeke, Mwera, Mkoa wa Mjini Mgharibi, na kuiba bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG).
Tukio hilo lilitokea asubuhi mwishoni mwa wiki na kusababisha polisi kuanzisha msako mkali.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamdan Hamad, alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kwamba polisi inaendelea na uchunguzi.
Silaha hiyo iliyokuwa na risasi 15, ilikuwa imeachwa katika kituo hicho wakati askari aliyekuwa zamu alipokuwa barabarani kushughulikia magari ya mizigo na abiria.
“Ni kweli tukio hilo limetokea na tunaendelea na uchunguzi na kuna mtu mmoja tumemkamata kuhusiana na wizi huo,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa katika eneo la Bububu baada ya kutakiwa kusimama akiwa na gari lake, lakini aligoma na baadaye alishuka na kukimbia.
Aliingia Mtaa wa Bububu Bamboo na kusababisha mtafaruku mkubwa.
Tukio la wizi wa silaha hiyo limezidi kutia hofu wananchi kwa vile limekuja siku chache tangu kuwapo kwa matukio matano ya uhalifu wa kutumia silaha katika mji wa Zanzibar.
Tukio la mwisho ni la mfanyabiashara, Mohammed Raza, ambaye alivamiwa na majambazi nyumbani kwake, lakini hawakuweza kuingia ndani baada ya kurushiana risasi na askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) wanaolinda nyumba hiyo.
Wimbi la ujambazi huo limesababisha vikosi vya SMZ kuanza kufanya kazi za ulinzi wa raia na mali zao, kazi ambazo kikatiba hutakiwa zisimamiwe na Polisi.
Askari wa vikosi vya KMKM, JKU na Valantia wenye silaha wamekuwa wakisimamisha magari ya abiria na mizigo na ya watu binafsi na kuyapekua huku baadhi yao wakiweka doria katika makutano ya barabara.
Hatua hiyo imepongezwa na baadhi ya wananchi kuwa inaweza kusaidia kukabiliana na vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha ambao umekuwa ukiibuka kwa kasi katika mji wa Zanzibar na vitongoji vyake.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, jana aliingia visiwani Zanzibar na kujifungia muda mrefu na viongozi wa polisi Zanzibar.
Pia alikutana na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha.
Mwema alitua Zanzibar kwa helikopta saa 3 asubuhi na kwenda Makao Makuu ya Jeshi hilo Zanzibar, Mtaa wa Ziwani.
Huyo ni kiongozi wa pili kuja Zanzibar ghafla tangu kuibuka kwa matukio hayo, ambayo yamesababisha kuuawa kwa Ofisa Usalama wa Taifa, Mohammed Bakar, na kuporwa kwa mamilioni ya shilingi.
Kiongozi wa kwanza alikuwa ni Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Mohammed Aboud Mohamed, ambaye alifika Zanzibar, na kusema serikali imeshaanza kuchukua hatua za kukabiliana na vitendo vya uhalifu.