RAIS Jakaya Kikwete, katika uamuzi ambao ni nadra kufanywa na viongozi wengi wa Afrika, ameamua kugharimia matibabu ya mmoja wa wapinzani wake kwenye nafasi ya urais, Anna Senkoro, wa Chama cha PPT - Maendeleo.
Anna aliugua kiharusi mwishoni mwa mwaka jana, na kumfanya afya yake itetereke.
Habari za kulipiwa matibabu hayo zilifichuliwa na Senkoro mwenyewe mwishoni mwa wiki wakati akihojiwa katika kituo cha televisheni cha Star.
Senkoro ambaye ni mwanamke wa kwanza nchini kuwania nafasi hiyo, alimsifu Rais Kikwete kwa kumwelezea kuwa ni mtu mwenye upendo, huruma na mchapa kazi.
Alisema bila msaada wa kiongozi huyo, angekuwa amekwisha kufariki dunia.
Alisema akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), alipata huduma zote muhimu kutokana na maagizo ya Rais Kikwete.
“Licha ya kuwa mpinzani wakati ule, Rais Kikwete ndiye aliyenigharimia katika matibabu.
“Amenisaidia sana, nilipokuwa Muhimbili nilipata vipimo vyote kama wanavyofanya kwa kiongozi wa serikali,” alisema.
Kuhusu mwelekeo wa vyama vya upinzani nchini, alisema vitaishiwa hoja kutokana na utendaji mzuri wa serikali ya Kikwete.
“Tangu alipoingia madarakani, Rais hatulii, hangoji kuletewa matatizo ya wananchi, anakwenda mwenyewe, ameshughulikia kila tatizo na kila hoja ya upinzani, mwaka 2010, hawatakuwa na hoja,” alisema Senkoro.
Senkoro alisisitiza umuhimu wa wapinzani kuungana, vinginevyo hawawezi kuingia Ikulu.
Senkoro kwa sasa ameachana na PPT na hajajiunga na chama chochote, ingawa dalili zinaonyesha kuwa ameanza kupiga jaramba litakalomwezesha kurejea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwenyekiti wa PPT - Maendeleo, Peter Mziray, alisema kitendo cha Rais Kikwete kumtibu mgombea huyo kilikuwa cha kumrubuni ili ajiunge CCM.
“Sitashangaa Mama Senkoro akijiunga CCM, kila siku tunaiambia serikali kama kweli ina nia njema na upinzani, kwa nini isitoe ruzuku kwa vyama vyote ili vyama vijiendeshe, ikiwa ni pamoja na kugharimia matatizo kama hayo ya viongozi wa upinzani?” alihoji.
Mziray alihoji sababu za serikali kutomtibu mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Jumbe Rajab Jumbe, ambaye kifo chake kilisababisha uchaguzi uahirishwe kwa mwezi mmoja na hivyo kuongeza gharama za uchaguzi.