Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Rais azuia leseni mpya za madini
Rais azuia leseni mpya za madini
By Habari Tanzania | Published  07/18/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Tamali Vullu, Dodoma

SERIKALI imesimamisha utoaji wa leseni kwa kampuni kubwa mpya zinazotaka kuwekeza katika sekta hiyo, Bunge limeelezwa.

Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Ibrahim Msabaha, alisema hayo jana alipokuwa akiwasilisha makadirio ya matumizi ya fedha ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2006/2007.

Kusitishwa kwa leseni hizo kumefanywa ili kutekeleza agizo la Rais Jakaya Kikwete, la kuundwa kamati inayodurusu mikataba ya madini.

Kamati hiyo imeundwa ili kuona uwezekano wa sekta hiyo kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Dk. Msabaha alisema taarifa ya awali imeshawasilishwa serikalini.

Alisema mojawapo ya mafanikio ya upitiaji upya wa mikataba ya madini ni kufikiwa kwa makubaliano kati ya serikali na kampuni za uchimbaji mkubwa wa madini kukubali kuanza kulipa dola 200,000 za Marekani kwa mwaka kwa halmashauri zenye migodi kama kodi.

“Malipo ya kodi hiyo kwa halmashauri yamekuwa hayafanyiki kwa kipindi kirefu kutokana na utata wa kisheria uliosababishwa na kupingana kwa mikataba ya madini na Sheria ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982.  

“Majadiliano yaliyofikiwa baina ya Serikali ya Awamu ya Nne na kampuni hizo yalifanikisha kupatikana kwa ufumbuzi wa utata wa kisheria uliokuwapo na hivyo kuruhusu malipo hayo ya kodi kwa halmashauri husika kuanza kufanyika.

“Hadi sasa Kampuni ya Barrick Gold Tanzania inayomiliki migodi ya Bulyanhulu, Tulawaka na North Mara imelipa sh 734,999,999 kwa wilaya za Kahama, Biharamulo na Tarime.

“Kampuni ya Resolute itaanza kulipa kodi kwa Halmashauri ya Nzega kuanzia Septemba, mwaka huu,” alisema.

Alisema baada ya kamati ya kudurusu sera ya madini kuwasilisha taarifa yake serikalini, wizara imebainisha maeneo muhimu na vipengele vya sera na sheria itakavyofanyiwa marekebisho.

Vipengele hivyo ni kuongeza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa kwa kuongeza fungamanisho la sekta ya madini na sekta nyingine.

Vipengele vingine ni taratibu za uwekezaji na vivutio kwa utafutaji na uchimbaji wa madini na ushiriki wa serikali kimkakati katika umiliki wa migodi.

Alisema sheria ya usonara itafanyiwa marekebisho kwa kufuta na kuongeza baadhi ya vipengele, ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kukuza uongezaji thamani ya madini.  

Akizungumzia suala la umeme, Dk. Msabaha, alisema katika kukabiliana na tatizo la nishati hiyo nchini, serikali imenunua mitambo ya kuzalisha megawati 100 itakayofungwa Ubungo, Dar es Salaam na mingine ya megawati 45 itakayofungwa Tegeta jijini humo.

Alisema hatua hiyo ni ya muda mfupi, na kwamba imechukuliwa na serikali ili kukabiliana na tatizo hilo nchini.

 Alisema kuwa mtambo wa Tegeta utatumia fedha za serikali na msaada kutoka Serikali ya Uholanzi.

Aliliambia Bunge kuwa serikali itakodi mitambo ya megawati 100 na kuifunga Ubungo.

Mitambo yote itazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia ya Songosongo na inatarajiwa kuanza kuzalisha nishati hiyo kati ya Novemba, mwaka huu na Julai, 2007.  

Alisema mpango wa muda wa kati wa kuongeza uzalishaji umeme katika gridi ya taifa ni kufunga mitambo ya gesi ya kati ya megawati 200 hadi megawati 300 eneo la Kinyerezi, Dar es Salaam ifikapo mwaka 2010.

Pia alisema mpango mwingine ni kutekeleza mradi wa Ruhudji wenye uwezo wa kuzalisha megawati 358 kwa kutumia nguvu ya maji ifikapo mwaka 2012.

Dk. Msabaha alisema kuwa wizara inakamilisha majadiliano na Kampuni ya Coal and Power Limited (KCP), ili kupanua uwezo wa kuzalisha umeme katika kituo cha Kiwira wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira na Kabulo.  

Alisema mkataba wa makusudio wa kuweka misingi ya uendelezaji wa mradi huo kati ya serikali, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na KCP ulisainiwa Machi, mwaka huu.

Mchakato wa kupata ridhaa ya serikali kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo, umeanza.

 Dk. Msabaha alisema mradi wa uunganishaji wa gridi za taifa za umeme za Zambia, Tanzania na Kenya umefikia hatua ya uendelezaji.

“Kikao cha mawaziri wa Nishati kilichofanyika Mei, mwaka huu, Mombasa, Kenya, ratiba ya uendelezaji  wa mradi iliidhinishwa.

“Mshauri mwelekezaji atakamilisha mchakato wa kutafuta fedha ifikapo Mei, 2007,” alisema.

Aliliomba Bunge limwidhinishie sh 465,202,173,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara na mashirika yaliyo chini yake.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.