Wawekezaji wote walioshindwa kuendeleza maeneo ya ardhi kwa ajili ya vitegauchumi Zanzibar, watanyang’anywa maeneo hayo.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Maji,Ujenzi, Nishati na Ardhi, Bw. Mansour Yussuf Himid wakati akifunga mjadala wa bajeti yake katika mwaka wa fedha 2006/07 kwenye kikao cha Baraza la Wawakilishi.
Bw Mansour alisema wawekezaji watakaoshindwa kuyaendeleza maeneo hayo, watanyang’anywa kuanzia mwaka ujao wa fedha.
Alisema Wizara yake tayari imewasilisha mapendekezo hayo serikalini na kwamba zaidi ya hekta 300 walizoshindwa kuziendeleza, zitanyang’anywa.
’’Serikali haitaruhusu kutoa ardhi kwa wawekezaji wanaoshindwa kuyaendeleza maeneo yao na wale ambao hawana fedha wasije,’’ alisisitiza Waziri Mansour.
Alisema ipo tabia kwa baadhi ya wawekezaji kuomba viwanja kwa ajili ya kuendeleza miradi, lakini baadaye hushindwa kufanya hivyo.
Aidha, alisema baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakikwepa kulipia ada ya ardhi.
Hata hivyo, alisema kuanzia sasa wawekezaji wa namna hiyo watabanwa ili kuhakikisha wanalipa madeni yao.
Na katika hatua nyingine, Waziri Mansour alisema serikali imekubali kuwapatia viwanja wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Pemba na Unguja baada ya kazi za upimaji kukamilika.
Alisema mradi wa uendelezaji ardhi Zanzibar (SMOLE) umeanza kupima viwanja katika maeneo mbalimbali.
Hata hivyo, alisema wajumbe kutoka Pemba watapewa Pemba na kutoka Unguja watapewa Unguja.