Mabaki ya mtu anayedaiwa kuuawa takriban miezi mitano iliyopita, yamekutwa katika kijiji cha Mbangamawe mkoani Ruvuma, kando kando ya barabara iendayo Njombe.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Falhum Mshana, alisema mabaki hayo yaligunduliwa baada ya raia wema kutoa taarifa polisi.
Kamanda Mshana alisema masalia yaliyokutwa eneo hilo ni fuvu la kichwa, mifupa na nguo za kike, jambo linaloashiria kuwa, marehemu huyo alikuwa ni mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kati ya 20 na 26.
Kadhalika, alisema katika eneo la tukio, ilikutwa damu iliyoganda ikiwa imetapakaa.
Kamanda Mshana aliongeza kuwa, uchunguzi wa awali uliofanywa na daktari umebaini kuwa, marehemu alifariki dunia takriban miezi mitano iliyopita.
Alisema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kwamba mpaka sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.