Seriakali imekubali kutoa dhamana ya dola za Marekani milioni 14 (sawa na Sh. bilioni 17), kwa ajili ya kusaidia kupunguza gharama za umeme utakaozalishwa na Mradi wa Uendelezaji Gesi ya Mnazi Bay.
Mradi huo upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Akizungumza jana na wakazi wa Manispaa ya Mtwara-Mikindani mara baada ya kutembelea mradi huo juzi mchana, Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa, alisema hatua hiyo itasaidia wakazi wa mikoa ya Kusini na hasa Lindi na Mtwara, wanunue umeme kwa bei sawa na Watanzania wengine.
”Serikali imetoa dhamana hiyo kwa vile inaamini itafungua mlango na kuchochea kuanzishwa kwa miradi mingine katika mikoa ya Lindi na Mtwara”alisema huku akishangiliwa na wakazi hao.
Alisema ziara yake inawathibitishia wananchi kuwa serikali ya Awamu ya Nne inaunga mkono mradi wa umeme wa Mnazi Bay kwa asilimia 100.
Aliwataka wakazi wa mikoa ya Kusini kutumia fursa ya umeme na barabara ya lami, inayoendelea kujengwa, kujieletea maendeleo kwa haraka.
’’Ninawaomba wakazi wa mikoa ya Kusini kutumia fursa za kuwepo kwa gesi na barabara ya lami, kuinua maisha yenu? muwahimize wajasiriamali wenu watumie vizuri fursa hizo ambazo zinakuja, msije kulalamika kuwa watu wa Msumbiji wametumia fursa hizo wakati nyie mnaziangalia,’’ alisema.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mkoani Mtwara kwa ziara ya siku moja, alifuatana na Waziri wa Nishati na Madini,Dk.Ibrahim Msabaha,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi), Bi. Hawa Ghasia, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bw. Mathias Chikawe, wabunge kutoka mikoa ya Mtwara na baadhi kutoka mkoa wa Lindi.
Kwa upande wake, mtaalamu wa mabomba ya gesi wa kampuni ya Artumas, Bw. Gregg Loades, alimweleza Waziri Mkuu kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu.
Alisema kazi ya kutandika mabomba ya gesi baharini, inatarajiwa kufanyika katika kipindi cha wiki sita kuanzia sasa.
Wakati akiwa njiani kuelekea Ruvula Camp na Likungu, ili kupata maelezo ya mitambo ya kuchuja na kusafirishia gesi, wanakijiji wa Mngoji wakiwa na mabango yao walisimamisha msafara wa Waziri Mkuu na kumweleza kero zao juu ya kutopatikana kwa dawa ya Sulphur ya kupulizia mikorosho.
Pia, wakati akirudi akitokea Kilindi kukagua bomba la gesi litakapopita kuanzia baharini hadi Mtwara mjini, kwenye mtambo wa kuzalisha umeme kutokana na gesi hiyo,alisimamishwa katika vijiji vya Msimbati na Ziwani, na kulazimika kuhutubia wakazi hao na kujibu kero zao.
Wakazi hao walizuia msafara wa Waziri Mkuu, huku wakiwa na mabango yaliyoeleza kuwa wananyimwa ajira na wamechosha kukatwa kodi za zao la korosho.
Baadhi ya mabango hayo yalisema ’’Sulphur hatukupata, haikuwafikia walengwa; mikopo haifiki kwa walengwa inaishia kwa viongozi’’.
Akijibu hoja kuhusu upatikanaji wa sulphur, Waziri Mkuu alisema mabango ya kuhitaji sulphur yamemfurahisha, kwa sababu yanaashiria maendeleo kwa kuwa anayedai dawa za kuua wadudu wa mazao ni sawa na mtu anayedai mbolea.
Alisema mabango hayo yametoa ujumbe kuwa kuna tatizo katika utekelezaji wa maamuzi ya serikali yaliyofikiwa katika kikao cha kujadili uendelezaji wa zao la korosho.
Alisema kikao hicho kilichoitishwa Mei mwaka huu, pamoja na mambo mengine, kilijadili suala la dawa za kupulizia mikorosho.
Alisema kufuatia ujumbe huo, alimwagiza Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Bw. Joseph Mungai, kwenda mkoani Mtwara kusimamia mbolea na dawa.