Kufuatia kuibuka kwa kasi kwa vitendo vya ujambazi wa kutumia silaha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ), sasa imeamua kuviingiza rasmi vikosi vyake vya SMZ. Vikosi hivyo ni pamoja JKU na KVZ.
Vikosi hivyo vimeanza kuimarisha ulinzi kwa saa 24 katika maeneo ya kibiashara na makutano ya barabara katika sehemu mbalimbali.
Hivi sasa askari hao wanaendesha doria katika sehemu mbalimbali, huku wakiwa wanatembea kwa vikundi mitaani.
Mbali ya kuweka ulinzi huo, askari wa vikosi hivyo wamekuwa wakiwapekua watu wanaowatilia mashaka na magari.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Bakari Khatib Shaaban, alisema operesheni maalum imeanzishwa na polisi kwa ushirikiano na vikosi vya SMZ tangu mfanyabiashara maarufu visiwani humu, Bw Mohammed Raza, avamiwe na majambazi yakiwa na silaha nyumbani kwake Kibweni, Unguja.
’’Serikali imeamua vikosi vishirikiane na polisi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu hasa ujambazi wa kutumia silaha,’’ alisema Kamanda Khatib.
Alifafanua kuwa lengo la operesheni hiyo ni kuongeza nguvu za ulinzi.
Hata hivyo, alisema askari wa vikosi watafanyakazi kwa maelekezo ya polisi, kwa vile ndio wanaofahamu sheria na masuala yote ya jinai.
Kamanda Khatib alisema tangu kuchukuliwa hatua hiyo, hali ya usalama katika Manispaa ya Zanzibar imerejea kuwa ya kawaida na taarifa za matukio ya ujambazi, zimepungua kwa kiasi kikubwa.
Kamanda huyo alisema ni kweli baadhi ya wananchi Zanzibar wamekuwa wakilalamikia usumbufu kutokana na vizuizi vilivyowekwa hasa nyakati za usiku.
Lakini, alisema hatua hizo zinachukuliwa kwa faida yao.
’’Tukubali kusumbuka kwa faida na usalama wa mali zetu, wananchi wasione kama kero gari moja kupekuliwa zaidi ya mara tatu,’’ alisisitiza Kamanda Khatib.