.Cheney: Watanzania mmechagua vema Rais
.Condoleezza Rice asema wana imani naye
Na Maura Mwingira, Washington
RAIS George Bush ameeleza kuridhishwa na kufurahishwa kwake kwa namna ambavyo Rais Jakaya Kikwete alivyoanza kazi ya kuongoza Tanzania.
Bush ametoa pongezi hizo wakati wa mazungumzo na Rais Kikwete, Ikulu ya Marekani (White House), yaliyohudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Marekani, Dicky Cheney, juzi.
"Nataka kutumia nafasi hii kukupongeza kwanza kwa kuchaguliwa kwako kuwa Rais wa Tanzania, lakini pia kueleza furaha yangu na kuridhishwa kwangu kwa namna ulivyopania kukuza uchumi wa nchi yako, kuendeleza utawala bora na kudumisha amani, si tu katika Tanzania, bali katika Afrika na dunia nzima," alisema Rais Bush.
Aliongeza kuwa, pamoja na Rais Kikwete kuanza vizuri na kuonyesha uhodari mkubwa katika miezi michache ya uongozi wake, lakini pia amekuwa mstari wa mbele kuendeleza uhusiano na ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania.
Rais Bush alisema Tanzania na Marekani zimekuwa zikishirikiana vizuri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, na akatumia nafasi hiyo kuipongeza Tanzania kwa kazi nzuri inayofanya katika Baraza hilo.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alimshukuru Rais Bush kwa pongezi na sifa alizompatia na kuongeza kuwa yuko nchini humo kwa lengo la kujitambulisha kwao na kwa wananchi wa Marekani kuwa yeye ndiye Rais mpya wa Tanzania.
Rais Kikwete aliwathibitishia viongozi hao nia yake thabiti ya kukuza na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya mataifa hayo mawili, yenye tofauti kubwa za kimaendeleo.
Baada ya kusalimiana na kutoa pongezi hizo kwa Rais Kikwete, Rais Bush aliondoka na kuwaacha Rais Kikwete na Makamu wa Rais Cheney wakiendelea na mazungumzo.
Mazungumzo kati ya viongozi hao wawili yalijikita katika kuangalia ni kwa namna gani mataifa hayo mawili yatakavyoweza kushirikiana na kusaidiana katika kukuza uchumi na kuendeleza ushirikiano.
Cheney alimweleza Rais kuwa serikali yake itaendelea kuisaidia Tanzania na kutoa ushirikiano mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta za uchumi, siasa na kijamii, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa Tanzania inafanikiwa katika juhudi zake za kupunguza umaskini.
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kumchagua kiongozi bora, makini na ambaye ameonyesha nia ya dhati ya kuwatumikia Watanzania.
Awali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Condoleezza Rice, ambaye alikuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu kukutana na kuzungumza na Rais Kikwete, alisema kuwa utawala wa Marekani una imani kubwa naye na unaridhishwa sana na uhusiano mzuri ulipo kati ya nchi hizo mbili.
Waziri huyo wa mambo ya nje alielezea kufurahishwa kwake kukutana na Rais Kikwete na kueleza kuwa fursa hiyo ilikuwa inafungua milango ya kukuza ushirikiano wa kiuchumi, kijamii, kisiasa na ulinzi na usalama kati ya mataifa hayo mawili.
Alitumia nafasi hiyo kumwomba Rais Kikwete kutumia ushawishi wake katika kuishawishi serikali ya Sudan kukubali majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa kwenda Darfur.
Allisema kuwa Marekani isingependa kuona kuwa majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa yanakwenda Darfur kama majeshi ya NATO, bali inachotaka ni ushirikiano na kufanya kazi pamoja na majeshi ya Umoja wa Afrika.
Condoleezza alimtaja Rais Kikwete kuwa ni kati ya viongozi wachache sana ambao wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa amani inatawala duniani kote.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kiwete aliishukuru serikali ya Marekani kwa misaada ya kiuchumi na kimaendeleo ambayo imekuwa ikiipatia Tanzania.
Pamoja na shukrani hizo, Rais aliiomba serikali ya Marekani, kuendelea kuisaidia Tanzania, hususani jeshi la polisi kwa kulisaidia vifaa na mafunzo ili liweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu, yakiwamo ya vita dhidi ya ugaidi.
Pia Kikwete aliiomba Marekani kuishawishi serikali ya Burundi kukaa meza moja na kikundi cha FNL PALIPEHUTU, baada ya serikali ya Tanzania kuwa imefanya kila lililowezekana kuishauri, lakini bila mafanikio.
Alisema Tanzania imefanya kazi kubwa ya kumshawishi kiongozi wa kundi hilo, Agaton Rwasa, kujitokeza na kukubali kuzungumza na serikali, lakini serikali ya Burundi imekuwa ikisuasua.
Kuhusu vita dhidi ya rushwa, moja ya mambo yaliyoikuna serikali ya Marekani, hasa kwa hatua mbalimbali anazochukua Rais katika kukabiliana nayo, Kikwete alisema kuwa hivi sasa serikali inaandaa taratibu za kisheria zitakazoiwezesha Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB) kutekeleza majukumu yake bila ya kuingiliwa na upande wowote, na bila woga.
Akiwa katika siku zake za mwanzo za ziara yake ya kikazi hapa Marekani, Rais Kikwete alipata pia fursa ya kupata chakula cha mchana kilichoandaliwa na maseneta wa Marekani, chakula ambacho kilihudhuriwa na masenata wenye sauti na ushawishi mkubwa katika serikali ya Marekani.
Baadhi ya maseneta wenye ushawishi mkubwa aliokula nao na kuteta nao ni Richard Luga, Thad Cochran na Barak Obama.
Rais pia alitazamiwa kukutana na viongozi wakuu wa Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF).