JAJI wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mbeya, ametupilia mbali maombi ya kupinga matokeo yaliyompatia ushindi Mbunge wa Jimbo la Kwela, Dk. Chrisant Mzindakaya (CCM).
Maombi hayo yalitolewa na upande wa mlalamikaji, lakini wanasheria walitumia vifungu batili vya sheria wakati wa kuomba kufutiwa ada ya sh milioni tano kwa ajili ya kufungulia kesi hiyo.
Kwa udhaifu huo wa kukosea vifungu husika, upande wa mlalamikiwa uliiomba Mahakama itupilie mbali malalamiko hayo.
Jaji alisema shauri hilo linaweza kurudishwa tena mbele ya mahakama hiyo endapo upande wa walalamikaji utakuwa na haja ya kuendelea nayo, lakini baada ya kutumia vifungu sahihi vya sheria kuhusu madai yao.
Akitoa uamuzi wa kesi hiyo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Chande Othman, alisema kuwa ameridhishwa na hoja za kisheria zilizotolewa na upande wa washitakiwa kwamba vifungu vilivyotumiwa na walalamikaji vilikuwa batili.
Jaji Othman alisema Mahakama imeshindwa kufanyia kazi maombi hayo yaliyokuwa mbele yake kisheria na kuona kana kwamba hakuna maombi yoyote mbele yake, hivyo kutupilia mbali kitu ambacho kipo mbele yake kimakosa ni uamuzi sahihi.
Alisema kifungu cha sheria namba 111(5b) kilitumika kimakosa katika maombi hayo, na kwamba kifungu sahihi kilikuwa ni cha namba 111(3) ambavyo vilitakiwa kwenda kwa pamoja katika kuomba kufutiwa ada ya sh milioni tano au kupunguziwa.
Jaji Othman alisema anakubaliana na wakili wa upande wa utetezi kwamba mbali na vifungu hivyo kutumika kimakosa, pia maombi yalipelekwa nje ya muda unaokubalika kisheria.
Alisema hoja iliyotolewa na upande wa utetezi kwamba kipindi hicho majaji wote walikuwa kwenye likizo ya Sikukuu ya Krismasi, si sahihi, kwa kuwa wakati wote mahakama zinakuwa wazi na kesi huendelea kusajiliwa na Msajili wa Mahakama.
Hata hivyo, alisema shitaka hilo linaondolewa mbele ya Mahakama kwa kuwa lipo kimakosa, na kwamba walalamikaji kama bado wana haja ya kuendelea na kesi hiyo, wanayo haki ya kuirudisha tena baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria.
Katika Uchaguzi Mkuu wa Desemba 30, 2005; Chama cha NCCR-Mageuzi kilipinga matokeo yaliyompatia ushindi Dk. Mzindakaya, ambaye anatetewa na Richard Rweyongeza.
Washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa ni Dk. Mzindakaya, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Wakili wa NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi, akizungumza kwa simu na Tanzania Daima, alisema anakusudia kuiwasilisha kesi hiyo upya mahakamani.