Serikali wilayani Kibondo imelipongeza shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa ushirikiano wake katika kupambana na umasikini na ujinga wilayani Kibondo.
Pongezi hizo zimetolewa jana na viongozi mbalimbali wa serikali wakati wa hafla fupi ya kumwaga aliyekuwa mkuu wa shirika hilo wilayani Kibondo Bw. Bayisa Wak Woya aliyemaliza muda wake.
Akihutubia katika sherehe hizo mkuu wa wilaya ya Kibondo Luteni Kanal John Mzurikwao amemtaja bw. Bayisa kuwa amekuwa kiunganishi kikubwa baina ya UNHCR na serikali pamoja na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake mratibu wa wakimbizi wa wilaya wizara ya mambo ya ndani Bw. Edward Machimu amebainisha kuwa kabla ya kuwepo kwa Bw. Bayisa UNHCR ofisi ya Kibondo haikuwa na ushirikiano na serikali.
Nao viongozi mbalimbali wa mashirika yanayohudumia wakimbizi na maendeleo vijijini kwa ufadhili wa UNHCR wameeleza kufurahishwa kwao na utendaji wa Bw. Bayisa na kumtaka kiongozi mpya wa UNHCR Bw. Abdlrahiman Issa kuiga mfano huo.
Bibi Nyinisaeri Gwamagobe mratibu wa shirika la Redesho ameyataja baadhi ya mafanikio ya kazi za UNHCR kuwa ni pamoja na ujenzi wa shule ya sekondari ya Gwanumbu, Mugombe, Biturana, Rubanga na Nyamtukuza.
Kwa upande wake Bw. Bayisa amekiri kuona uchungu wa maendeleo kutokana na kwamba yeye amekuwa ni mkimbizi akiwa na miaka 18 na kwamba anapoona wananchi wanahangaika haoni sababu ya kutosaidia.
Amefafanua kuwa ufadhili uliotolewa si wake binafsi bali ni ufadhili wa UNHCR na kusisitiza kuwa suala la elimu ni muhimu sana ili watoto wapate elimu jirani na nyumbani.
Amemtaka pia anayechukua nafasi yake Bw. AdulRahiman Issa kuiga mfano wake kwa kujenga mahusiano mazuri na serikali pamoja na wanachi bila kuwasahau wakimbizi.
Naye Bw. Rahman ameahidi kufuata nyayo za mtangulizi wake na kwamba hakuja kuharibu mahusiano bali kujenga umoja na kuendeleza mapambano dhidi ya umasikini na kuwasaidia wakimbizi
Bw. Bayisa Wak Woya ambaye ni raia wa Sweden mzaliwa wa Ethiopia amekuwa mkuu wa UNHCR Kibondo tangu Mei mwaka 2004.