Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Benki ya Dunia yasema Tanzania nchi ya mfano
Benki ya Dunia yasema Tanzania nchi ya mfano
By Habari Tanzania | Published  07/15/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu
 
TANZANIA imetajwa kuwa ni mfano wa kuigwa na nchi nyingine za Afrika kutokana na kutumia misaada yake vizuri kama inavyokusudiwa.
 
Rais wa Benki ya Dunia Paul Wolfowitz alimweleza Rais Jakaya Kikwete jana Ikulu mjini Dar es Salaam alipokutana naye.
 
“Madhumuni yangu kuja nchini na kutembelea nchi zingine Afrika ni kuona jinsi misaada ya Benki inavyotumika… hapa Tanzania nimeona misaada imetumika vizuri, ahadi zimetekelezwa na nitakapofika St. Petersburg (Russia) kwenye mkutano wa nchi tajiri nane duniani (G8), nitawaeleza mafanikio niliyoyaona hapa Tanzania,” Wolfowitz amemueleza Rais Kikwete.
 
Mapema, akimkaribisha Rais huyo wa Benki ya Dunia, Rais Kikwete alimweleza kwa kifupi juhudi za serikali katika kukuza uchumi, utawala bora na hali ya kisiasa kwa jumla.
 
“Kwa mara ya kwanza makusanyo yetu ya kodi yamevunja rekodi, kwani tumekusanya kiasi cha sh. bilioni 226.348 na tunaona uchumi wetu unazidi kukua,” alisema Rais.
 
Kikwete aliongeza kuwa katika hali ya kisiasa, serikali inafanya juhudi kubwa katika kutatua matatizombali mbali ya kisiasa, hasa upande wa Zanzibar ambapo tatizo kubwa liko katika mgawanyo wa kisiasa kati ya Pemba na Unguja.
 
“Umoja wetu wa kitaifa ni jambo kubwa sana ambalo tunajivunia tangu enzi za Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, hivyo hali ya kisiasa huko Zanzibar ni suala linalonigusa, kwani likiachwa jinsi lilivyo linaweza kuwa chanzo kikubwa cha vurugu kama hatulitatui kwa makini,” alisema Rais.
 
Alisema na kuongeza kuwa mbali na vyama vya siasa, pia anapanga kukutana na vikundi vya kijamii (NGOs) ili kuwahakikishia kuwa anauthamini mchango wao katika jamii.
 
Naye Wolfowitz alisema amefurahishwa sana na umoja na utulivu uliopo hapa Tanzania na kueleza alivyofurahia ziara yake katika maeneo mbalimbali hapa nchini, hasa katika kitongoji cha Manzese ambapo ameona watu wanajituma na kufanya biashara kwa utulivu na umoja bila kubaguana kiitikadi.
 
Mapema akiwa Manzese, Rais huyo wa Benki ya Dunia, alieelezea kufurahishwa kwake na jinsi Watanzania, hasa wa kipato cha chini walivyo na ari na moyo wa kuchangia katika kujiletea maendeleo yao.
 
Aliyaeleza muda mfupi baada ya kuzindua mradi wa maji safi na salama, katika kitongoji cha Manzese kwa Mfuga Mbwa, ikiwa ni moja ya sehemu aliyotembea mjini Dar es Salaam kujionea miradi ya uboreshaji wa miundombinu katika makazi yasiyopangwa kwa kuishirikisha jamii.
 
Miradi hiyo ilianzishwa mwaka 2001 kwa madhumuni ya kuinua hali ya maisha ya wananchi katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, inaendeshwa chini ya programu shirikishi kupitia mkopo wa sh. bilioni nane (sawa na asilimia 90 ya gharama zote) kutoka benki hiyo.
 
Akizungumza katika eneo hilo huku akiwa amezungukwa na umati wa wakazi hao, Wolfowitz aliwashukuru wananchi hao kwa mchango wao wa asilimia tano ya fedha katika kufanikisha miradi hiyo.
 
Wolfowitz alisema kitendo hicho kimedhihirishia na kutoa sura mpya kwa benki hiyo kuwa hata watu masikini wanaweza kuchangia katika kuleta maendeleo.
 
Pia, katika eneo hilo, Wolfowitz, alijionea shughuli za ujenzi wa barabara wa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 1.86 inayoanzia barabara kuu ya Morogoro, eneo la Tip Top hadi makutano ya barabara ya Mabibo.
 
Miundombinu mingine inayojengwa chini ya mradi huo ni mifereji, vifaa vya taka na taa za barabarani kwa upande wa Manispaa ya Kinondoni.
 
Kwa upande wa Manispaa ya Temeke, barabara ya Sandali inayojengwa kwa kiwango cha changarawe yenye urefu wa kilomita 2.8. Pia, itakuwa na taa za barabarani na vifaa maalum vya kuthibiti taka.
 
Kata zingine zitakazoboreshwa chini ya programu hiyo, ni Kigogo na Mwananyamala katika Manispaa ya Kinondoni, Buguruni na Vingunguti katika Manispaa ya Ilala na Chang’ombe, Keko na Azimio katika Manispaa ya Temeke.
 
Chini ya programu hiyo ambayo Jiji na Halmashauri zake zinachangia pia asilimia tano, zaidi ya barabara 19 zinatarajiwa kujengwa na kuboreshwa katika kata tano za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam.
 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa eneo hilo wameelezea kufurahishwa kwao na uboreshaji wa miundombinu hiyo, hasa maji ambayo ndiyo kilio kikubwa katika maeneo hayo ya Manzese.
 
Pia, Rais huyo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi mbalimbali ambao hawakusita kuelezea furaha na kilio chao kwa huduma za maji.
 
Fatuma Said (32) mama wa watoto wanne alimueleza Wolfowitz, juu ya tatizo la maji katika eneo hilo ambayo hupatikana visimani.
 
Alisema maji hayo yana chumvi na kwamba yale ya kutoka bombani ni ghali, kwani huuzwa kati ya sh. 300 na sh. 400.
 
Naye Wiston Emmanuel (23) ambaye ni fundi cherehani katika eneo hilo, alisema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo, hasa barabara kutarahisisha mawasiliano na hatimaye kuongeza idadi ya wateja.
 
Katika ziara yake hiyo, Wolfowitz aliongozana na Meya wa Jiji la Dar es Salaam Adam Kimbisa na Mwakilishi Mkazi wa Benki hiyo, Judy O’connor.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.