Kanisa lashindwa kumpata mkuu mpya
Dk. Mushemba kuendelea kukalia kiti
Na Omari Shaaban, Arusha
PAMOJA na wajumbe kurudia kupiga kura mara tatu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limeshindwa kumpata mkuu wake mpya wa kuliongoza kutokana na mchuano mkali kati ya wagombea.
Uchaguzi ulifanyika usiku wa kuamkia jana ambapo wagombea wa nafasi hiyo walishindwa kupata idadi ya kura zilizokuwa zinahitajika ‘kunyakua’ uongozi huo.
Kutokana na kushindwa kwa uchaguzi huo, Mkutano Mkuu wa KKKT, saa tisa usiku uliamua kwa kauli moja kumuidhinisha kiongozi aliyemaliza muda wake Askofu Dk. Samson Mushemba, aendelee kuliongoza kanisa hilo kwa mwaka mmoja, huku wakijipanga kwa uchaguzi mwingine.
Uchaguzi huo ambao ulifanyika kwenye Ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Makumira uligubikwa na makundi, ndani ya wagombea hao, na hali hiyo ndiyo iliyoelezwa na baadhi ya wajumbe kuwa chanzo cha kushindwa kumpata Mkuu mpya wa kanisa hilo.
Kabla ya kuanza mchakato huo, wagombea ambao ni Askofu Dk. Owdenburg Mdegella (Dayosisi ya Iringa) na Askofu Dk. Stephen Munga (Kaskazini Mashariki), walitolewa nje na kujadiliwa na wajumbe hao na kisha kuingia ndani na kuanza mchakato huo wa kuwania uongozi wa juu kabisa wa kanisa hilo.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi huo na mwongozo wa katiba ya KKKT, ili kushinda ni lazima mgombea apate theluthi mbili ya kura zote ambapo idadi ya wapiga kura wote ilikuwa 179. Hakuna mgombea aliyefanikiwa kupata kiwango hicho cha kura ambazo ni 119.
Kwenye uchaguzi huo ambao ulianza saa 4:37 usiku, katika matokeo ya kwanza yalikuwa kura 89 kwa 86. Kwa kufuata kanuni za uchaguzi za KKKT, Mwenyekiti wa Mkutano huo, Askofu Dk. Mushemba hakutaja ni nani aliyepata idadi ipi, bali aliwatangazia wajumbe kwamba hakuna mgombea aliyepata theluthi mbili, na hivyo kulazimika wajumbe kurudia kupiga kura.
Uchaguzi ulirudiwa na katika matokeo yalipotangazwa saa sita usiku, Askofu Mushemba alisema kura zilikuwa 90, kwa 84, na kura mbili ziliharibika na hakukuwa na mshindi, na hapo hapo maombi yakaanza, kwa ajili ya duru ya tatu ya kupiga kura.
Katika duru ya tatu, wagombea hao walipata tena kura 91 kwa 85, na kura moja iliharibika na hivyo uhitimisha upigaji kura.Kufuatia hali hiyo, mkutano mkuu ulikaa tena na kujadili mustakabali wa kumpata kiongozi wa kuongoza kanisa hilo, hivyo kuamua kumuidhinisha Askofu Dk. Mushemba kushika wadhifa huo tena kwa mwaka mmoja.
Baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu huo, wakitoa maoni yao baada ya uchaguzi huo, kwa waandishi wa habari walisema kuwa hali hiyo inatakona na mgawanyiko uliosababishwa na migogoro ya mara kwa mara iliyolikumba kanisa hilo hivi karibuni.
Walisema miongoni mwa migogoro hiyo ni kutenganishwa Dayosisi ya Same ili ipatikane dayosisi ya Mwanga, kushtakiwa kwa maaskofu saba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa KKKT, Amani Mwenegoha na mingine ya ndani kwa ndani bila ya kufafanua zaidi.
Siku mbili kabla ya uchaguzi huo, Waziri Mkuu Edward Lowassa, alipofungua mkutano, aliwaasa wajumbe kuacha makundi na kuchagua Mkuu wa Kanisa ambaye atakuwa kichocheo cha maendeleo na umoja kwenye kanisa.
Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa KKKT, Brighton Kilewa, mkutano ulimchagua Exaud Ndullu kuwa mwandishi wa KKKT kwa kipindi cha miaka minne. Ndullu ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, anachukua nafasi ya Seth Kitange ambaye amemaliza muda wake.