Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Uozo Maliasili
Uozo Maliasili
By Habari Tanzania | Published  07/15/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:
Diallo aambiwa kaza moyo, umekula kiapo
 
Msindai ataka kamati maalum kugawa vitalu
 
Na Esther Mvungi, Dodoma
 
WABUNGE kadhaa wameilalamikia Idara ya Wanyamapori kwa utendaji mbovu na kumtaka Waziri wa Maliasili na Utalii ajidhatiti kuikabili hali hiyo.
 
Walisema kutokana na utendaji wake usioridhisha, usiokuwa wa uwazi, mapato yanayopatikana kutoka Idara hiyo ni kidogo ikilinganishwa na rasilimali inayovunwa.
 
Mbunge wa Iramba Mashariki Mgana Msindai (CCM), alisema suala la watu kuhamishwa na kukataa limeigawa Idara ya Wanyamapori kwamba wapo wengine ambao ni watu wa mkurugenzi.
 
Alisema iundwe Tume kushughulikia suala hilo akisema kama Jeshi la Polisi limefanya uhamisho ni kwa nini Idara ya Wanyamapori kuwe na matatizo.
 
Msindai alisema endapo Tume itaundwa mapato yatokanayo na wanyamapori yataongezeka maradufu kuliko ilivyo sasa.
 
Alisema watendaji wamekuwa wakikaa ofisini na kutokwenda kwenye maeneo yao ya kazi, hivyo amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Anthony Diallo kujizatiti kupambana na hilo.
 
“Waziri jizatiti kupambana na hilo, utapigwa vita lakini umekula kiapo kufanya kazi,” alisema Msindai.
 
Alisema iundwe kamati maalum ya kugawa vitalu vya uwindaji na uwepo ukomo wa uwindaji katika vitalu hivyo, kwa kuwa wananchi wamekuwa wakishindwa kupata maeneo ya uwindaji.
 
Alisema wawindaji wengi ambao ni wa kigeni wamekuwa wakisema wamepewa maeneo kwa miaka 29 na kuhoji kuwa hayo ni makoloni yao?
 
Msindai alisema wawindaji hao wa kigeni wamekuwa wakipata mapato makubwa wakati nchi inachopata ni robo tu ya mapato yao.
 
Mbunge wa Kahama James Lembeli alisema kwamba Idara ya Wanyamapori lazima itupiwe macho,kwani mambo mengi yamekuwa yakifanyika na kuzua utata katika jamii.
 
Alisema hakuna uwazi katika mapato yanayotokana na utalii katika idara hiyo, na kutoa mfano kwamba, mtalii akipanda Mlima Kilimanjaro analipa kama dola za Marekani 50 au dola 60, lakini akiwanda nyati gharama yake haifahamiki.
 
“Watu wanaona ndege zinaingia na kutoka, usimamizi hakuna… hakuna anayefahamu ni kiasi gani cha fedha kinaiingia,” alisema na kuongeza: “Panapofuka moshi pana moto.”
 
Akaonya kwamba iwapo hatua za haraka za kudhibiti mapato yatokanayo na wanyamapori hayatadhibitiwa, lengo la sekta ya utalii kuchangia katika pato la taifa zaidi ya asimilia 16 hadi angalau kufikia asilimia 20 itakuwa ndoto.
 
Alihoji pia kwamba, inakuwaje Waziri anamhamisha mfanyakazi wa wizara yake halafu anagoma kuhama, wakati wengine wakihamishwa hukubali.
 
Nayo Kamati ya Bunge ya Maliasili na Mazingira imeeleza kusikitishwa na uhamisho wa watumishi wa Idara ya Misitu na Wanyamapori ambao hautekeleziki.
 
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mbunge wa Kongwa Job Ndugai (CCM), alitoa masikitiko alipokuwa akitoa
 
taarifa ya kamati kuhusu utekelezaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii katika mwaka wa fedha 2005/06 na
 
maoni juu ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2006/07.
 
Ndugai alisema suala hilo limeipaka matope wizara machoni pa wananchi.
 
Katika hatua nyingine, Ndugai alisema Kamati ya Maliasili na Mazingira imetoa maoni kwa serikali
 
ikisisitiza umuhimu wa kuwasilishwa bungeni muswada wa sheria mpya ya wanyamapori kabla ya mwisho wa mwaka huu.
 
Pia, imeshauri kuundwa kwa wakala mpya utakaoshughulikia masuala ya uwindaji wa kitalii ili
 
kutoa fursa kwa Idara ya Wanyamapori kushughulikia sera, sheria na uhifadhi kwenye mapori ya akiba na hifadhi za wananchi.
 
Ndugai alisema kamati inapendekeza serikali iongeze viwango vya ada na tozo mbalimbali kwa kampuni za uwindaji wa kitalii, kwa vile rasilimali iliyopo ambayo inavunwa hailingani na mapato yanayopatikana
 
ikilinganishwa na nchini nyingine za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
 
Mbunge wa Viti Maalumu Magdalena Sakaya (CUF), akitoa maoni ya kambi ya upinzani alisema suala la mkurugenzi wa wanyamapori kung’ang’ania kuendelea kukaa kwenye nafasi hiyo linatia doa serikali ya Rais Jakaya Kikwete.
 
“Hakuna mtu mwenye mali na cheo, mbona maofisa wengine wa wizara hiyo waliokumbwa na ‘hamishahamisha’ hiyo waliondoka wakati nao pia wameteuliwa na Rais? Kunani katika kiti chake?” alihoji Magdalena.
 
Alisema kutokana na hali hiyo ya watu kugomea maofisini kama ilivyo hivi sasa TANAPA ambako baadhi ya maofisa wanapanga kwenda mahakamani kupinga kuhamishwa, inadhihirisha kwamba kuna maofisa waandamizi serikalini wanaomlinda.
 
Magdalena alisema matatizo ndani ya Idara ya Wanyamapori yamewafanya baadhi ya wafadhili kama
 
shirika la GTZ la Ujerumani kujitoa kwenye ufadhili.
 
Magdalena kwa upande wake alisema serikali iangalie upya Sheria ya Wanyamapori ya Mwaka 1974 ili kuwepo chombo kitakachoangalia utaratibu na leseni za maeneo ya uwindaji zitakavyotolewa na mapato yake yatakavyodhibitiwa.
 
Akitoa mchango wake, Mbunge wa Ukerewe Balozi Getrude Mongella (CCM), alisema Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa haipewi fedha inayostahili kuhimili mahitaji yake na pia alitoa rai kwa wizara itangaze vivutio vingine vya utalii vilivyopo nchini ambavyo havijatangazwa.
 
Katika hatua nyingine, Balozi Getrude alisema suala la wavuvi wadogo halijaangaliwa kwa umakini akitaka wavuvi hao walindwe na kupatiwa mfuko wa ajili ya kuwaendeleza.
 
Mbunge wa Hai Fuya Kimbita (CCM), alipongeza hatua ya wizara ya kufuta vibali vya uvunaji wa magogo akisema kuwa walikuwapo wavunaji wa kigeni ambao kwa kutumia vifaa vya kisasa walikuwa wakisababisha nchi kuwa jangwa.
 
Kwa upande wao, Mbunge wa Jang’ombe Mohammed Rajab Soud (CCM) na Mbunge wa Mafia Abdulkarim Shah (CCM) waliiomba wizara kuruhusu kuuzwa kwa magogo yaliyokatwa na watu waliokuwa wamepewa vibali.
 
Walisema watu hao walikuwa wameomba mikopo benki na wanashindwa kuirejesha.
 
Mbunge wa Viti Maalumu Savelina Mwijage (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu Mwanawetu Zarafi (CUF) na Shah walisema wavuvi wadogo wamekuwa wakisumbuliwa na maofisa wa maliasili kwa kutumia nyavu zisizoruhusiwa, lakini pia wamekuwa wakiwaacha wavuvi wakubwa wanaotumia meli kutumia nyavu hizo.
 
Mbunge wa Ngorogoro Kaika Telele (CCM), alisema Wamasai wamekuwa wahifadhi wazuri wa wanyamapori kwa kipindi kirefu na kuiomba serikali kufanya makubaliano nao wanapowaondoa kwenye hifadhi badala ya kuwaeleza tu ondokeni.

How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.