POLISI mkoani Dar es Salaam, inamsaka daktari wa kike wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa tuhuma za kuandika ujumbe (SMS) wa matusi kwa mke wa wakili wa kujitegemea (jina limehifidhiwa).
Polisi imefikia hatua ya kumsaka daktari hiyo baada ya mke wa wakili huyo kutoa malalamiko hayo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Afred Tibaigana, alisema jana kuwa mke wa wakili huyo amefungua kesi yenye namba OB/RB/11740/06 katika kituo cha polisi cha Oysterbay na taarifa hizo kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi.
“Ni kweli tumepata malalamiko, na meseji hizo za matusi na kashfa tumezisoma, kwa bahati nzuri daktari huyo anatumia mtandao wa Tigo, kwa hiyo tunafuatilia kuweza kujua ni nani na anapatikana wapi,” alisema Tibaigana.
Hata hivyo, habari ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa daktari huyo anadaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wakili huyo.
“Tunamwita wakili huyo tuzungumze naye, tujue kama kweli wana uhusiano na daktari huyo, na yeye atatusaidia kumpata kwani hatutarajii kwa mwanamke huyo msomi awe na tabia hiyo,” alisema Tibaigana.
Alipohojiwa na Tanzania Daima, mke wa wakili huyo alisema anahisi daktari huyo ana uhusiano wa kimapenzi na mumewe.
Alisema ni kawaida kwa daktari huyo kumtukana na kumtishia kwamba ataachika na yeye atachukua nafasi yake.