TAASISI ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), imemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuirudisha Tanzania kwenye uanachama wa Jumuia ya Uchumi ya nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) ili kujenga uchumi bora wa nchi.
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Elvis Musiba, wakati alipokuwa akifunga warsha ya siku moja ya wadau mbalimbali wa mambo ya uchumi, katika Hoteli ya Movenpick iliyokuwa inajadili athari za Tanzania kujitoa uanachama kwenye jumuiya hiyo.
“Tunamuomba Rais Jakaya Kikwete atumie busara zake zote kuhakikisha Tanzania inarudi tena kuwa mwanachama wa COMESA ili tuweze kujenga uchumi wa nchi, hasa kwa wenye viwanda,” alisema Musiba.
Alisema si kweli kwamba viwanda vingi nchini vimeshindwa kuuza bidhaa katika soko la COMESA kwa madai kuwa viko chini ya viwango vinavyohitajika kimataifa.
Musiba alisema nchi zote zilizoko kwenye Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika (SADC) ni wanachama wa COMESA, hivyo itakuwa jambo la aibu kwa Tanzania kujitoa, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwafungia wafanyabishara soko lao.
Alisema siku zote Rais Kikwete amekuwa mstari wa mbele kuzitaka taasisi zisizokuwa za kiserikali na wamiliki wakubwa wa viwanda kuhakikisha wanakuwa mbele katika kupandisha uchumi wa Tanzania.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara Afrika Mashariki (EABC), Arnold Kilewo alisema umefika wakati sasa wa Tanzania kuamua mambo yake kwa ajili ya manufaa ya watu wake.
Alisema kutegemea soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki peke yake halitaisaidia zaidi kama bidhaa nyingi zinazozalishwa hapa nchini hazitasafirishwa nje ya nchi