RAIS wa Benki ya Dunia, Paul Wolfowitz, ameahidi kusaidia tatizo la umeme linalozikabili nchi za Afrika Mashariki, ambalo linachangia kushuka kwa uchumi kwa nchi za ukanda huo.
Alisema hayo jana kwenye mkutano wake na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), uliofanyika katika Hoteli ya Coffe Lodge, iliyopo nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Alisema kuwa Benki ya Dunia inaahidi kusaidia Jumuiya hiyo ili kufanikisha malengo yake.
Alisema mbali ya kusaidia tatizo hilo, Benki ya Dunia itajitahidi kuona namna ya kupata njia mbadala na kuondoa tatizo hilo la umeme ambalo kwa muda mrefu limekuwa likiwaumiza vichwa viongozi wa nchi hizo na kuleta athari za kiuchumi.
Pia ameahidi dunia kuimarisha EAC katika masuala mbalimbali ya kibiashara, ushuru wa forodha na kuona namna gani wanavyoweza kushiriki mazungumzo ya amani ya nchi ya Burundi.
Rais huyo pia ameahidi kujikita katika vita dhidi ya ugonjwa wa malaria, ugonjwa ambao umekuwa ukiteketeza maisha ya watu wa nchi zinazoendelea na kuona namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.
“Tupo tayari kusaidia maendeleo hayo iwapo viongozi wa nchi za Afrika Mashariki kama viongozi hawatakuwa na utashi wa kisiasa. Tupo pamoja nanyi kuwasaidia ili muondokane na kero mbalimbali,” alisema.
Awali, Rais huyo alikuwa na mazungumzo ya faragha na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, katika Hoteli ya Coffee Lodge, na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali walimwomba awaeleze kilichozungumzwa kati yake na Rais huyo wa Benki ya Dunia.
Hata hivyo, Mkapa aligoma kuzungumzia walichojadili katika mazungumzo yao na kuishia kusema: “Mazungumzo yangu na Rais wa Benki ya Dunia yalikuwa ya faragha na ninaomba yaendelee kuwa ya faragha kama tulivyozungumza.”
Rais huyo wa Benki ya Dunia amekwenda mkoani Dodoma ambako anatarajiwa kuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, baadhi ya mawaziri, wenyeviti wa kamati ya fedha na uchumi, huduma za jamii, na hesabu za serikali. Baada ya ziara hiyo atakwenda jijini Dar es Salaam ambako atakutana na Rais Jakaya Kikwete