Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mawaziri vivuli waleta sokomoko barazani
Mawaziri vivuli waleta sokomoko barazani
By Habari Tanzania | Published  07/14/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, amesema kuanzia sasa hotuba za mawaziri vivuli atazikagua kabla ya kuwasilishwa, ili kuondoa maeneo yanayolenga uchochezi.

Kificho alitangaza uamuzi huo baada ya Waziri Kivuli wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Hamad Masoud, kuwasilisha maoni ya kambi ya upinzani ya wizara hiyo.

Spika Kificho alisema ameamua kuchukua uamuzi huo kutokana na baadhi ya mawaziri vivuli kuutumia Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi kama jukwaa la kisiasa.

“Naona mnaendelea kuleta hoja zile zile ambazo tumekataza, kuanzia sasa hotuba nizione mapema, ili kuangalia kama zinaruhusika au hapana,” alisema Kificho.

Aliwaeleza wajumbe kwamba pale atakapoona hotuba inakwenda kinyume na kanuni za Baraza, hataruhusu isomwe hadi hapo itakapohaririwa na kutolewa maeneo yasiyofaa.

Spika alisema kwamba haiwezekani Ukumbi wa Baraza hilo ukaanza kutumiwa na baadhi ya wajumbe kwa kazi za siasa, na kuwataka mawaziri vivuli kuzingatia na kuheshimu kanuni.

“Pamoja na kwamba utaratibu huu si mzuri, lakini kwa faida ya Baraza na wananchi nitalazimika kuziangalia,” alisema.

Alisema kwamba lazima kanuni za Baraza zizingatiwe, ili kuepusha kanuni zisizokuwa na msingi, na ndiyo maana amekuwa akiwakumbusha wajumbe mara kwa mara kusimama kwenye hoja iliyo mbele yao.

Mapema, Spika Kificho alimuweka kitako Waziri Kivuli wa Wizara hiyo ya Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Hamad Masoud, baada ya kuanza kutoa shutuma dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuwa walifanya dhuluma katika uchaguzi uliopita.

“Mheshimiwa, hebu kaa kwanza, naomba urudi katika hoja inayojadiliwa, kama utaendelea kuzungumza mambo yaliyokuwa nje ya hoja, nitakatisha hotuba yako na kukutoa nje ya ukumbi,” alionya Kificho.

Akiwasilisha maoni ya kambi ya upinzani, Masoud alisema anampongeza Rais Jakaya Kikwete, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, na anaamini CCM haitaongozwa tena kibabe na itasita kutumia vyombo vya dola kukiendesha, kukidumisha na kitaheshimu katiba na sheria za nchi.

Hata hivyo, alisema katika uchaguzi uliopita wananchi wa majimbo 16 ya Unguja walifanyiwa dhuluma kubwa kutokana na njama za ZEC na kutumiwa kwa vyombo vya dola.

Aliyataja majimbo aliyodai yamefanyiwa hujuma hizo kuwa ni Mpendae, Amani, Magomeni, Bububu, Mtoni, Matemwe, Mwanakwerekwe, Fuoni, Magogoni, Nungwi, Rahaleo, Bumbwini, Tumbau, Kiembesamaki na Dimani.

Alisema kwamba vitendo vya dhuluma vinavyofanyika Zanzibar katika uchaguzi ndivyo vinavyowafanya wananchi waishi maisha magumu.

“Si kiangazi wala mvua kubwa, si kushuka wala kupanda kwa bei za bidhaa duniani, si tsunami wala Catrina, lakini ni dhuluma iliyokithiri ifikapo uchaguzi mkuu, ndiye mchawi wa Zanzibar,” alisema Masoud.

Mapema, akiwasilisha bajeti yake, Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, Mansour Yussuf Himid, aliwapongeza Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume; Rais Kikwete; na Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohammed Shein, kwa kuchaguliwa na wananchi kuiongoza nchi.

Alisema kitendo cha wananchi kumchagua Rais Karume kwa mara nyingine kinaonyesha imani kubwa aliyonayo kwa wananchi ya kuwaongoza na kuwaletea maendeleo.

Baada ya kikao hicho kuahirishwa saa 1:45 usiku, Spika Kificho; Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha na vigogo wengine walikutana katika ukumbi wa mapumziko na kuwa na mazungumzo marefu. Kilichozungumzwa hakijafahamika


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.