Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Cheyo: Serikali imejaa vikongwe
Cheyo: Serikali imejaa vikongwe
By Habari Tanzania | Published  07/14/2006 | Habari za Kitaifa | Rating:

MBUNGE wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), amesema serikali imejaa watumishi wazee kwa kuwa wanaogopa kustaafu kutokana na masilahi duni wanayolipwa kama mshahara wakiwa kazini, na hivyo kuathiri pensheni yao.  

Alisema watumishi wengi serikalini ni wakongwe waliopaswa kuwa wamestaafu, lakini kila muda wao ukiwadia wanaomba wapewe kazi ya mkataba kwa vile kustaafu hakuna tija.  

“Tuna serikali nzee... serikali ya vikongwe...mababu wanafanya kazi na wajukuu,” alisema.

Cheyo alisema hayo jana alipokuwa akichangia hotuba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Utawala Bora; Siasa na Uhusiano wa Jamii, iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.  

Cheyo alisema mshahara hauwasaidii watumishi, na kwamba wengi wanaponea kwenye marupurupu na posho za safari nje ya ofisi; na akasema kwamba marupurupu hayo ni makubwa kuliko mishahara.  

Alisema kwa utaratibu wa sasa, hata ongezeko la mishahara halitawasaidia wafanyakazi kwa kuwa watakaofaidika na posho hizo ni wakubwa.  

“Baya zaidi, allowance hazimsaidii mtumishi mdogo, hazikatwi kodi, na ndiyo maana pensheni ya wastaafu ni ndogo,” alisema.

Cheyo alipendekeza serikali iweke viwango rasmi vya mishahara, ili kuleta motisha kwa watumishi, badala ya sasa ambako mfanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wa Wizara kama ya Nishati na Madini; na Wizara ya Afya wanapishana mno kipato.

Ili kuwasaidia wafanyakazi, alisema, ni vema serikali iongeze posho hizi katika mishahara, ili ziwafaidishe wadogo na wakubwa, na zitunishe pensheni ya mstaafu.

Aliungwa mkono na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyeikosoa serikali kwa kupandisha mishahara kizamani katika Sikukuu ya Wafanyakazi au kila inaposoma bajeti mpya.  

Hamad Rashid alishauri serikali iweke mfumo wa kudumu wa kutambua ufanisi wa watumishi wake na kuwaongezea mishahara au kuwapandisha vyeo kila inapobidi kisheria.

Alisema asilimia 15 hadi 50 zilizoongezwa sasa hazina maana, kwa kuwa hazionekani, na akashauri posho ziongezwe katika mshahara kwa sababu kadhaa.  

Kwanza, alisema, serikali inaogopa kuingiza posho hizo kwenye mshahara kwa sababu haitaki kuwalipa wafanyakazi pensheni nono; lakini alionya kwamba kwa kutoingiza posho hizo, serikali inajiibia, kwa kuikosesha kodi ambayo ingekatwa.

Tatu, serikali inapunguza muda wa watumishi kukaa ofisini kufanya kazi, kwani watalazimika kusafiri au kuwa kwenye semina nje ya ofisi, ili kujiongezea posho.  

Wote wawili, Cheyo na Hamad Rashid, walimtaka waziri anayeshughulikia siasa na uhusiano wa jamii, Kingunge Ngombale-Mwiru kutoka ‘mafichoni’ na kuonyesha programu ya kazi ya namna ya kumaliza migogoro ya kisiasa nchini, hasa Zanzibar.

“Kingunge alete programu yake, tujue nini kilichoandaliwa,” alisema Hamad Rashid.

Alisisitiza kuwa bila waziri huyo kuwajibika sasa, kuna hatari migogoro ya kisiasa ikamomonyoa utulivu na amani tunayojivunia.

Cheyo alimshauri Kingunge kutumia Tanzania Centre for Democracy kama uwanja wa mazungumzo ya kisiasa kuhusu masuala tete, kwa kushirikisha vyama vyote.  

“Kingunge ajihusishe na mikutano ya wanasiasa...ndiyo namna ya kumsaidia rais...ili siasa itumike kujenga nchi,” alisema Cheyo.

Mawaziri wahusika na wizara hizo walitarajiwa jana kuhitimisha mjadala kwa kujibu hoja za wabunge.

Mawaziri hao ni Ghasia (Menejimenti ya Utumishi wa Umma); Kingunge (Siasa na Uhusiano wa Jamii) na Philip Marmo (Utawala Bora).


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments
  • Comment #1 (Posted by ana)
    Rating
    sawa kabisa cheyobadala ya kusihafu wewe unamteua kuwa balozi wakati umri umekwisha
     
Submit Comment


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.