INSPEKTA Jenerali wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, amewaonya polisi wanaojifanya kuwa ni ‘mabosi’ wa wananchi.
Alisema hayo juzi mjini hapa kwenye Ukumbi wa Mkapa alipokuwa akiwaelezea wananchi umuhimu wa kuanzishwa kwa mfuko wa umma wa kupambana na vitendo vya uhalifu mkoani hapa.
Alisema polisi hawawezi kuwa mabosi wa wananchi isipokuwa wanapaswa kuwa watumishi waaminifu na watiifu kwa wananchi kwa kuwa ndio wenye uwezo wa kumchagua rais na kumuweka madarakani.
Alisema polisi wanafanya kazi ya kuwatumikia wananchi na kamwe hatafurahi kusikia kuwa wao ndio mabosi wa wananchi, kwa kuwa hata yeye alichaguliwa na rais ambaye alipata madaraka hayo kwa ridhaa ya wananchi.
“Polisi hatuwezi kuwa mabosi wa wananchi isipokuwa polisi wanapaswa kuwa watumishi wa wananchi,” alisisitiza IGP Mwema.
Alisema kazi kubwa iliyopo mbele ya jeshi hilo ni kusimamia ulinzi wa raia na mali zote na kwamba mafanikio makubwa yatapatikana endapo wananchi watakuwa tayari kutoa ushirikiano mkubwa kwa jeshi hilo na kazi hiyo ni ile ya kuwafichua wahalifu kwa kuwa wapo ndani ya jamii.
Aliwataka wananchi, hususan wafanyabiashara wa mkoani hapa, kujitolea kwa hali na mali katika ulinzi na kuchangia mfuko wa umma, kwa kuwa hao ndio waathirika wa kwanza na kwamba wahalifu wote huwatupia macho kwa mali walizonazo.