NI ajabu na kweli. Hirizi imedaiwa kugeuka na kubainika kwamba kumbe alikuwa ni kijana aliyefariki dunia miaka mitatu iliyopita.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana na kuzusha gumzo zito kwa wakazi wa Jiji la Mbeya na kusambaa kwa kasi.
Tukio hilo linadaiwa kufanywa na mkazi wa Kijiji cha Msaleche - Mtwango, kilichopo mkoani Iringa.
Akiwa katika stendi ya mabasi ya Mwanjelwa jijini hapa, mwananchi huyo aliyetambuliwa kwa jina la Mzee Kinyagano Mlelwa, aliyekuwa anasafiri kutoka Iringa kwenda Mbeya kumtafuta ndugu yake, alidondosha kwa bahati mbaya hirizi hiyo.
Mmoja wa watu walioshuhudia tukio hilo, John Asubisye, alisema kuwa baada ya gari alilokuwa anasafiria mzee huyo kufika katika kituo cha mabasi cha Mwanjelwa, Mlelwa aliingiza mkono mfukoni mwake akitaka kutoa pesa. Badala ya kutoa pesa, alijikuta akitoa hirizi, kitu kilichowashangaza baadhi ya abiria.
Akaambiwa amedondosha ‘mzigo wake’. Alipoangalia chini, akawataka watu wote waliokuwapo hapo wafumbe macho, lakini karibu watu wote walikataa kufumba.
Asubisye alisema kuwa baada ya mzee huyo kuona watu wanagoma kufumba macho hadi waelezwe sababu za kufanya hivyo, aliinama kuiokota akiwa anatetemeka.
Alisema alipoigusa, ghafla ilitokea fimbo, na kwamba wakati wakiwa bado hawajaelewa kinachoendelea, fimbo hiyo iligeuka, akaonekana mtu.
“Hapo tulichanganyikiwa na kuanza kutimua mbio huku na kule, ndipo watu wengine wakaja mbio upande wetu ili kushuhudia nini kimetokea katika gari hilo.
“Baada ya muda, polisi walifika na kumwokoa mzee huyo ambaye wananchi walikuwa wanataka kumshambulia wakimtuhumu kuwa ni mshirikina,” alisema.
Inadaiwa kuwa baadhi ya ndugu wa mzee huyo waliofika katika tukio hilo, walimtambua kijana huyo anayedaiwa kuibuka kutoka katika hirizi kuwa ni Herman Mlelwa; mtoto wa pili wa mzee huyo ambaye anadaiwa alifariki dunia miaka mitatu iliyopita.
Mzee na mtoto huyo walipelekwa polisi huku umati mkubwa wa watu ukifuatilia tukio hilo.
Kijana huyo alikuwa hazungumzi, na baadhi ya watu wanaodadisi masuala ya ushirikina, walisema alikuwa amechukuliwa ‘msukule’.
Mmoja alidai kwamba alikuwa amekatwa ulimi, ndiyo maana alikuwa hawezi kuzungumza.
Tukio hilo lilimlazimu Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Moshi Chang’a, kuingilia kati.
Chang’a, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, alitoa ufafanuzi kwa maelfu ya wananchi katika Kituo Kikuu cha Polisi kuwa tukio hilo limegubikwa na utata na kwamba serikali inaendelea na uchunguzi.
Hata hivyo, Chang’a alisema kuwa tukio la hirizi kugeuka kuwa mtu ni uzushi na kwamba lilizushwa na watu wanaomfahamu mzee huyo.
Alisema watu waliokuwapo stendi, ndio waliozusha taarifa za hirizi kugeuka mtu.
“Tumemhoji mzee mwenyewe, hata yeye anakiri kuwa kulikuwa na vitendo vya kishirikina kuhusiana na mtoto wake na kwamba alikuja Mbeya kwa ajili ya kumtafuta ndugu yake ili amsaidie kuhusiana na tatizo hilo la mtoto wake,” alisema Chang’a.
Kiongozi huyo alisema tukio zima limejaa utata, hali inayoifanya serikali kwa kutumia vyombo vyake, ianze kulichunguza.
Chang’a, akimkariri mzee huyo, alisema aliwaeleza kuwa mtoto wake alipelekwa katika Hospitali ya Peramiho ambako alifanyiwa upasuaji na kutolewa masikio ya kuku mwilini pamoja na vitu vingine.
“Lakini tulipomchunguza mtoto, hana alama yoyote mwilini inayoonyesha amewahi kufanyiwa upasuaji,” alisema.