Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 11 wanaokabiliwa na kesi ya kuua wafanyabiashara watatu na dereva teksi, wametinga kortini tena leo huku wakiwa chini ya ulinzi mkali.
Askari kibao wa kikosi cha kutuliza ghasia, FFU, almaarufu kama vijana wa kazi, wamemwagwa eneo la mahakama ya hakimu mkazi Kisutu.
Alasiri imeshuhudia vijana wa kazi wakiwa wamejipanga katika viwanja vya mahakama huku wakiwa tayari tayari.
Kesi hiyo ilipangwa kutajwa leo wakati ilipoahirishwa kwa mara ya mwisho katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi.
Kabla ya kuahirishwa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Charles Kenyella alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hata hivyo baada ya mwendesha mashtaka kutoa maelezo hayo, baadhi ya washtakiwa walinyoosha mikono na kuiomba mahakama iwaruhusu kutoa upya maelezo yao au kuandika maelezo ya nyongeza.
Washtakiwa walioomba kuandika maelezo ya nyongeza ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Ahmed Makelle, Konstebo Noel, Koplo Jane Andrew, Koplo Nyangelera E 6712 Felix Cedrick, Konstebo Michael na Koplo Rashid Lema.
Hata hivyo, Zombe na wenzake watatu D 2300 Abeneth, Koplo Rajabu na Koplo Emmanuel Mabula hawakuomba kuchukuliwa maelezo yao.
Baada ya maombi hayo, Afande Kenyella alimuomba hakimu muda wa kufanya mawasiliano akidai kuwa jalada halisi halipo mikononi mwa polisi, na kwamba liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Hakimu Mwengesi alikubaliana na washtakiwa na kuwapa ruksa ya kufanya kama walivyoomba.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa mnamo Januari 14, mwaka huu, katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kumuua Ephraim Chigumbi.
Mwendesha Mashtaka alidai katika shtaka la pili kuwa, siku ya tukio la kwanza, katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, washtakiwa walimuua Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo.
Katika shtaka la tatu, ilidaiwa kuwa, siku ya tukio la kwanza na la pili, kwenye eneo la tukio la kwanza na la pili, washtakiwa walimuua Juma Ndugu.
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa, siku ya tukio la kwanza, pili na la tatu, katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, washtakiwa walimuua Mathias Lukombe.
Hata hivyo, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji