Watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wakiwa na silaha, wamevamia nyumba ya mfanyabiashara maarufu wa Zanzibar, Bw. Mohammed Raza na kurushiana risasi na askari wa Kikosi cha JKU, waliokuwa wakilinda nyumba hiyo.
Purukushani hizo zilizotokea usiku wa kuamkia jana, nyumbani kwa mfanyabiashara huyo Kibweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Majambazi hayo yalizidiwa nguvu na askari hao wa JKU, hivyo yakalazimika kutelekeza bunduki, aina ya Sub Machine Gun (SMG)ikiwa na risasi tano na kutimua mbio.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw. Bakari Khatib Shaaban, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Hata hivyo, Kamanda Bakari aliomba apewe muda zaidi kuzungumzia mazingira ya tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Bw. Raza alisema majambazi hayo yalivamia yakiwa na gari aina ya Isuzu Escudo.
Alisema baada ya kufika nyumbani kwake, yalizunguka ukuta na jambazi moja liliingia ndani.
Alisema tukio hilo lilitokea saa 9:00 usiku na kwamba askari wawili wa JKU waliyaona majambazi hayo na kuanza kufuatilia nyendo zao.
’’Mlinzi wakati akiwa juu ya ghorofa, alianza kuweka silaha sawa, lakini majambazi yaliposikia akijiandaa kwa kufyatua risasi, ndipo yalipoanza kuwarushia risasi walinzi,’’ alisema Bw. Raza.
Aliongeza kuwa na walinzi nao walijibu mapigo.
Alisema risasi moja iliyorushwa na majamabazi, ilipiga ukuta na katika purukushani hizo, yalizidiwa nguvu na kuamua kuibwaga chini bunduki yao na kutimua mbio.
’’Mwenyezi Mungu bado ananipenda, leo hii mngeamka mkasikia mambo mengine, na hii ni mara ya pili kuvamiwa na majambazi,’’ alisema Bw Raza.
Bw. Raza aliiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuruhusu wafanyabiashara kumiliki silaha, ili waweze kujihami wanapokabiliwa na matatizo kama hayo.
Alisema jambo la msingi ni kuwepo kwa utaratibu mzuri kuhakikisha wafanyabiashara wanaopewa silaha hizo ni waaminifu na wanaoheshimika.
Wakati huo huo, majambazi mengine yamefanikiwa kupora Sh. milioni 16, zikiwa mali ya kampuni ya uwakala wa bia ya One Stop Centre.
Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita.
Habari zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio, zilisema majambazi hayo yaliingia katika ghala lililopo mtaa wa Mkele Wilaya ya Unguja Mjini na kupora fedha hizo zilizokuwa zimehifadhiwa katika kasha la fedha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bw Bakari Khatibu Shaabani, alithibitisha tukio hilo na kusema polisi wanaendelea na uchunguzi.
Hilo ni tukio la tano la ujambazi wa kutumia silaha kutokea katika kipindi cha wiki moja katika Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika tukio la hivi karibuni, Ofisa mmoja wa Usalama wa Taifa, Mohammed Bakari Chenda, aliuawa baada ya majambazi kuvamia duka moja la kubadilishia fedha za kigeni.
Kufuatia mfululizo wa matukio hayo, Naibu Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Mohammed Aboud, alifanya ziara ya ghafla Zanzibar na kuahidi kuimarisha ulinzi mkali kukabiliana na uhalifu huo.
Hata hivyo, Waziri Aboud alisema bado ni mapema kwa Zanzibar kuruhusu watu binafsi kumiliki silaha.
Uchunguzi umegundua kwamba walinzi wengi wa jadi hutumia silaha za kienyeji, ikiwemo panga, visu na marungu.