Hatma ya majengo mawili yenye urefu wa ghorofa saba yaliyojengwa kinyume cha sheria za mipango miji, mali ya kampuni ya kampuni ya Empire Properties Ltd, Wajidali Jiwahirji ya jijini Dar es Salaam haijajulikana
baada ya viongozi wa Manispaa Kinondoni kukataa kuzungumzia suala hilo.
Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni juzi iliamuru majengo hayo yaliyopo makutano ya Barabara ya Toure Drive na Mwaya, Masaki, Dar es Salaam, yabomolewe.
Manispaa ya Kinondoni tayari imeuvunjavunja ukuta unaozunguka majengo hayo, ambayo yanadaiwa kujengwa kinyume na sheria za mipango miji.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Bw. Hassan Katanga, alikataa kuzungumzia suala hilo na alipopigiwa simu alikuwa akiikata bila kusema chochote.
Alipopigiwa simu na kuulizwa suala hilo, alikata simu haraka bila kutoa maelezo yoyote, ingawa viongozi wengi walisema yeye ndiye mwenye maelezo sahihi.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Bodi ya Uhandisi, Bw. Stephen Mlote, alisema bodi yake haina cha kusema kuhusu ubomoaji wa majengo hayo na alishauri atafutwe Waziri wa Miundombinu au Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni.
’’Kwa hilo sisi hatuna cha kuzungumza, majibu sahihi yanaweza kutolewa na Waziri wa Miundombinu na hasahasa mtafute mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni,’’ alisema Bw. Mlote.
Naye Msajili wa Bodi ya Makandarasi, Bw. Boniface Muhegi, alipofuatwa kuzungumzia suala hilo, alisema anajiandaa kwa safari ya Iringa na kwamba hana muda wa kuzungumza na waandishi wa habari.
’’Bosi anatoka sasa hivi kuelekea Iringa kikazi kwa hiyo anasema hana nafasi labda uje Jumatatu anaweza kuongea na wewe,’’ alisema Katibu Muhtasi wake.
SOURCE: Nipashe