a Mwandishi Wetu
WAFANYAKAZI wa hoteli ya Sea Cliff, iliyopo Masaki, Dar es Salaam, walirejea kazini juzi jioni na kuanza kutoa huduma.
Wafanyakazi hao, ambao waligoma kuanzia juzi asubuhi na mabosi wao, wengi wao wakiwa wazungu na wahindi, kulazimika kutoa huduma kwa wateja, wamerejea kazini kwa sharti kwamba menejimenti itekeleze madai yao ndani ya siku tatu tangu juzi.
Kwa walio zamu ya jioni walianza kazi saa 11 jioni na wenye zamu ya asubuhi walirudi nyumbani.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Hoteli na Nyumbani (CHODAWU), Peter Sakarani, alisema jana kuwa mwafaka huo ulifikiwa baada ya kufanyika kikao cha pamoja baina ya menejimenti, wafanyakazi na ofisa kazi wa mkoa. Hakumtaja jina.
Alisema, ofisa kazi aliwashauri waendelee na madai yao wakiwa kazini na ndipo walipokubali kurejea kazini.
Sakarani alisema kuwa madai ya wafanyakazi yamo ndani ya mkataba wa hali bora ya kazi walioingia na menejimenti Desemba, 2004 na yalianza kutekelezwa Machi 2005.
Kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye mkataba wa hiari, wafanyakazi wanadai walipwe malipo ya ziada wanapofanya kazi kwa saa za ziada, mazingira bora ya kazi na kulipwa malimbikizo waliyoahidiwa.
Sakarani alisema kuwa, Meneja Mkuu Kelvin Stander ameahidi kutekeleza madai yaliyomo chini ya mamlaka yake na yaliyo nje ya uwezo wake, atamsubiri Mkurugenzi wa hoteli, Shubash Patel aliyeko nje ya nchi.
Pia, alisema imegundulika kwamba menejimenti ilikwepa kusajili mkataba wa hali bora ya kazi katika Mahakama ya Kazi, kama inavyohitajika kisheria.
“Hata hivyo Ofisa Kazi alitufafanulia kwamba kama mmefikia makubaliano na baada ya miezi mitatu, hakuna upande uliodai mabadiliko yoyote, basi mkataba unakubalika kisheria,” alisema Sakarani, akiwa na maana mkataba uliopo unakubalika kisheria.
Wakati wafanyakazi wakiwa wamerejea kazini, menejimenti jana ilikuwa ikiendelea na kikao chini ya usimamizi wa ofisa kazi kujadili suala la mgomo huo.
Alisema wafanyakazi hao, sambamba na makubaliano ya jana, waliunda kamati ya wawakilishi 16 watakaofuatilia utekelezaji wa madai yao, ikiwemo marekebisho ya mkataba wa sasa kama ilivyoshauriwa kutoka kwenye kikao cha juzi.
Sakarani alidokeza kuwa, miongoni mwa maudhui ya jana ni kumhoji na kumjadili kiongozi mmoja wa hoteli, aliyedaiwa kumpiga na kumjeruhi mfanyakazi Yunus Kashakala.
Kiongozi huyo wa CHODAWU, alisema menejimenti juzi ilichukua hatua ya kugharamia matibabu ya mfanyakazi aliyejeruhiwa
Mara zote waandishi wa habari walipotaka kuzungumza na Meneja Mkuu Kelvin Stande kupata maoni yake, aligoma katakata kwa madai kwamba “ametingwa na kazi” na hata alipobanwa zaidi, alidai angezungumza na vyombo vya habari baada ya kikao.
Hadi saa 8.00 mchana, kikao kilikuwa hakijamalizika.
Sea Cliff ina jumla ya wafanyakazi 326, kati yao wageni wakiwa 17.