Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Jamhuri ya Watu wa China anayehusika na Utawala Bora, Qu Wanxiang, anatarajiwa kuwasili leo nchini kwa ziara ya siku nne.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa mjini Dar es Salaam jana na Ikulu ilisema ziara hiyo inafuatia mwaliko aliopewa na aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Wilson Masilingi, alioutoa wakati alipotembelea China mwaka 2004.
Akiwa nchini atafanya mazungumzo na Waziri anyeshughulikia Utawala Bora, Philip Marmo, atakwenda Zanzibar kuzungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mambo ya Katiba na Utawala Bora), Ramadhan Abdalla Shaaban na atatembelea Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB).
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge Duniani wa Kupambana na Rushwa (GOPAC) na mbunge wa Canada, John Williams, amesema kuwa hakuna nchi duniani ambayo haina tatizo la rushwa.
“Rushwa ipo katika kila nchi, hakuna nchi inayoweza kutamba kwamba hakuna rushwa, iwe tajiri au masikini, tofauti inakuja katika ukubwa wa tatizo na namna nchi inavyokabiliana nalo,” alisema Williams alipokuwa akizungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo. Mazungumzo hayo yalifanyika jana Ikulu.
Williams alisema kuwa Tanzania ni nchi mojawapo ambayo imefanya juhudi za wazi za kupambana na rushwa.
Alisema ni kutokana na juhudi hizo na utayari ulioonyeshwa na viongozi wa juu serikalini, kwa kushirikiana na wabunge na wadau mbalimbali, ndiyo maana GOPAC imeamua mkutano wake wa kimataifa ufanyike Tanzania.
Kwa upande wake, Marmo alisema serikali na Bunge watahakikisha kuwa wanatoa msaada wa hali na mali kuhakikisha mkutano huo wa kwanza kufanyika Afrika unafanikiwa.
Alisema Hazina tayari imetenga sh. bilioni moja kwa ajili ya mkutano huo utakaofanyika Arusha, Septemba, mwaka huu.
Alisema mtandao wa wabunge wa Afrika wa mapambano dhidi ya rushwa (APNEC), ambao yeye alikuwa mmoja wa wanzilishi wake, ulianzishwa kwa lengo la kuwahamasisha wadau mbalimbali, ikiwemo serikali, kuhusu mapambano dhidi ya rushwa.
Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Samuel Sitta, amesema kuwa Tanzania bado ina kazi kubwa ya kuweka utaratibu na mipaka ya gharama za uchaguzi kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Sitta alisema hayo juzi wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano GOPAC.
Utiaji saini huo ulifanyika kati ya mwenyekiti wa GOPAC, ambaye pia ni mbunge wa bunge la Canada, John Williams, na Spika Sitta kwenye ofisi za bunge mjini Dar es Salaam na kuhudhuria na Balozi wa Canada nchini, Andrew McAlister na baadhi ya wabunge.