Na Omari Shaaban, Arumeru
WAZIRI Mkuu Edward Lowassa amewataka wajumbe wa mkutano mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), kuhakikisha wanamchagua askofu atakayedumisha amani, mshikamano na upendo ndani ya kanisa hilo na siyo atakayekuwa kama ugonjwa wa polio katika utendaji wake wa kazi.
Lowassa aliwataka wajumbe ambao wapo kwenye mkutano wao mkuu wa 17, kujiepusha na migawanyiko yoyote itakayoweza kuukumba uchaguzi huo.
Mkutano utamchagua askofu mpya wa kuliongoza kanisa hilo baada ya wa sasa, Askofu Samson Mushemba, kumaliza muda wake keshokutwa.
Akizungumza jana kwenye ufunguzi wa mkutano huo, unaofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini, kilichopo Makumira wilayani Arumeru, Waziri Mkuu alisema kuwa katika uchaguzi mbalimbali wa kisiasa kunakuwepo na migawanyiko ya makundi, lakini hiyo haipaswi kujitokeza katika uchaguzi wa kidini, kutokana na kugusa imani zaidi badala ya siasa.
Waziri Mkuu alisema kuwa madhehebu ya dini na asasi zake yanafanya jitihada kubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo, ikiwemo kujenga shule, huduma za matibabu, shughuli za maendeleo ya kawaida kama upatikanaji wa barabara, maji na utunzaji wa mazingira.
Lowassa, ambaye pamoja na kufungua mkutano pia alizindua chuo hicho kikuu kishiriki, alisema kuwa uzinduzi huo ni kielelezo tosha cha mchango wa makanisa, katika maendeleo ya taifa, hususan katika sekta ya elimu.
Alisema vyuo vikuu vinapaswa kujiimarisha katika mafunzo na kufanya utafiti mbalimbali na kusambaza matokeo yake kwa jamii, kwa lengo la kuwaondolea wananchi umaskini.
Serikali, alisema, inatambua umuhimu wa mchango wa sekta binafsi katika kukuza elimu nchini, na kwamba mpaka sasa Tanzania ina vyuo vikuu vya umma na binafsi vinavyofikia 30, vyenye wanafunzi 36,870, na asilimia 14 ya wanafunzi hao wapo kwenye vyuo vikuu binafsi.
Waziri Mkuu alisema kuwa KKKT hapa nchini imekuwa mstari wa mbele katika kuchangia sekta ya elimu, na mpaka sasa ina shule za sekondari zaidi ya 50, za ufundi zaidi ya 20, vyuo vya ualimu viwili na chuo kikuu kimoja chenye vyuo vishiriki vitatu.
Leo Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, anatazamiwa kutoa mada kwenye mkutano huo kuhusu utandawazi na uwekezaji.