Na Premi Kibanga, Cape Town
BILIONEA wa Marekani Bill Gates ameahidi ushirikiano na Tanzania katika masuala ya elimu, afya na teknolojia ya habari.
Gates, ambaye ni Mwenyekiti wa kampuni ya kimataifa ya Microsoft, alitoa ahadi hiyo jana mjini hapa, alipokuwa na mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete na hatimaye kutiliana saini makubaliano hayo.
Makubaliano hayo yalitiwa saini katika kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Cape Town, ambapo wote wawili wanahudhuria semina iliyoandaliwa na Gates kwa ajili ya viongozi wa kiserikali, wafanyabiashara na wataalamu mbalimbali wa teknolojia ya habari.
Pia Rais Kikwete na Gates walizungumzia maeneo yenye umuhimu mkubwa, likiwemo la kusaidia Chuo Kikuu cha Dodoma kinachotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.
"Tungependa utupe msaada mkubwa, hasa katika hatua ya awali kabisa ya kujenga Kitivo cha Teknolojia ya Habari katika chuo chetu kipya kikuu cha Dodoma ambacho tunapenda kiwe kituo cha mawasiliano katika nchi, si za Afrika Mashariki tu, bali na za Maziwa Makuu kwani tupo katikati ya nchi hizi zote," alisema Rais Kikwete.
Maeneo mengine ambayo Rais Kikwete alimtaka bilionea huyo kusaidia ni katika mawasiliano ya kisasa katika sekta mbalimbali zikiwemo za elimu, afya, utalii na shughuli za kiserikali.
"Tungependa shughuli zetu za serikali pia tufike mahali tuwe tunazifanya kwa njia ya kisasa zaidi, maana kama tutafika mahali mtu anaweza kuomba pasi ya kusafiria, hati mbalimbali za serikali kwa njia hii ya mawasiliano ya kisasa, tutapunguza urasimu na pia kupunguza rushwa kwani mawasiliano na mikataba yote itakuwa wazi na ya haraka," alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumzia hilo, Gates alimhakikishia Rais kwamba anapenda kushirikiana na nchi za Afrika, hasa katika masuala ya elimu, afya na teknolojia.
"
Ni vizuri tukaanza majadiliano haraka iwezekavyo tuone ni kiasi gani kinahitajika na tunaweza kushirikiana vipi na akina nani katika hili, " alisema Gates na kumshukuru Rais Kikwete kwa kumualika kutembelea Tanzania.
"Ninapenda sana kuja, na bila shaka nitakuja kutembelea Tanzania. Mara ya mwisho nilikuja kama mtalii mwaka 1995, nilifurahi sana , napenda sana ziwa Tanganyika," alisema Gates.
Jana jioni pia Rais Kikwete alipata fursa ya kukutana na Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton ambaye pia ameahidi ushirikiano katika suala la Chuo Kikuu cha Dodoma.
Mkutano wa Microsoft unamalizika leo mchana ambapo Gates na Clinton watazungumza na baadaye watazungumza na washiriki juu ya teknolojia muhimu na ushirikiano na Afrika.