Afanikisha kuondoa makundi Tanga
Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi mkoa wa Tanga kimesema kuwa Katibu Mkuu Yussuf Makamba tangu aanze ziara yake mkoa wa Tanga amekuwa tiba ya maradhi sugu ya makundi ndani ya CCM.
Taarifa ya katibu wa CCM mkoa wa Tanga, Stephen Msami aliyoitoa jana kwenye vyombo vya habari ilikuwa ikipinga taarifa iliyotolewa na gazeti moja la kila siku (siyo Uhuru) kwamba ‘Makamba amekuwa shubiri kwa CCM’.
Msami alisema kuwa kufuatia ziara ya Makamba ambayo ni ya kwanza tangu ashike wadhifa huo mwezi uliopita imekuwa ya mafanikio kwa kuondoa makundi yaliyozuka baada ya kura za maoni katika kuwatafuta wagombea wa CCM kwenye uchaguzi wa mwaka jana.
Alisema Katibu Mkuu ametibu maradhi sugu ya makundi ndani ya CCM katika wilaya zote ambako amefanya ziara.
“Makundi yamezikwa na sasa mshikamano na uongozi wa pamoja umerejea kutokana na kazi nzuri ambayo kiongozi wetu ameifanya mkoani,” ilisema taarifa ya Msami kwa vyombo vya habari .
Alisema, Makamba, alihimiza mshikamano na uongozi wa pamoja na kwamba kiongozi au mwanachama anayeendekeza makundi hana nafasi ndani ya CCM.
“Alihimiza kufanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kazi ya Chama ndani ya Chama, na kazi ya Chama ndani ya umma likiwemo suala la usimamizi wa utekelezaji wa Ilani, uhamasishaji umma ili ushirikiane na serikali katika utekelezaji wa Ilani,” alisema Msami.
Msami alisema Katibu Mkuu pia alihimiza kazi za Chama zifanyike kwa ufanisi wa hali ya juu ikiwemo kuelimisha umma dhidi ya upotoshwaji unaofanywa na vyama vya upinzani.
Akizungumzia upotoshwaji uliofanywa na gazeti hilo, alisema siyo kweli kwamba Katibu Mkuu alitamka kuwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa hawawajibiki, hivyo wajiuzulu ili watoe nafasi kwa wengine wenye uwezo wa kutimiza majukumu yao vizuri.
“Kimsingi, habari hiyo ni upotoshaji wa ukweli na uzushi mtupu uliotolewa na waandishi wenye makusudi yao binafsi ya kuwagonganisha viongozi wa Chama na serikali,” alisema Msami katika taarifa yake.
Alisema mkutano uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mazoezi, Katibu Mkuu hakuwataja Wakuu wa Wilaya wala Wakuu wa Mikoa kwa suala lolote.
Msami alisema katika mkutano huo walijitokeza kina mama wawili mmoja alilalamikia suala la kukatwa minazi yake tisa bila fidia hata baada ya kufuatilia kwa muda mrefu.
Mama wa pili alilalamikia kuwa chakula cha njaa hakijagawanywa kwa wakazi wa mji wa Korogwe na alijieleza kuwa yupo katika hali mbaya ya njaa.
Alisema kufuatia maelezo ya mama huyo, Katibu mkuu alimuonea huruma mlalamikaji na akatoa fedha ili mama huyo anunuliwe gunia moja la mahindi.