KUNDI la majambazi limevamia duka la kubadilishia fedha za kigeni mjini Zanzibar na kumuua Ofisa Usalama wa Taifa na kupora mali na fedha taslimu.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Kathib Shaaban, jana alisema kwamba majambazi hao walivamia duka la mfanyabiashara, Nassor Mohammed Msumari, na kupora sh milioni tatu na kadi za simu zenye thamani ya sh milioni 12.
Kamanda Khatib alisema tukio hilo lilitokea saa 4 usiku wa kuamkia jana wakati mmiliki wa duka hilo akifanya biashara huku akiangalia mashindano ya Kombe la Dunia na baadhi ya wapita njia katika eneo la Darajani mjini Zanzibar.
Kamanda Khatib alimtaja Ofisa Usalama aliyeuawa kuwa ni Mohammed Bakar Chendwa. Alitarajiwa kuzikwa jana mjini Zanzibar.
Alisema majambazi hao walikuwa na silaha aina ya SMG na bastola moja. Baada ya kwenda katika duka hilo kama watazamaji wa mpira, ghafla waliwabadilikia wenzao na kufyatua risasi mfululizo.
Alisema baadaye majambazi hao waliwataka kusalimisha mali na vitu vya thamani.
Kamanda huyo alisema kwamba Ofisa Usalama aliyekuwapo katika eneo hilo alijaribu kuwazuia majambazi hao kwa kuziba barabara kwa kutumia gari lake, ndipo alipopigwa risasi kichwani na baadaye kufariki dunia wakati akipelekwa Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Alieleza kwamba pamoja na kuwa hakuna sheria ya muda kwa wafanyabiashara kufunga maduka, mfanyabiashara huyo alikiuka taratibu za kiusalama, kwa kukaribisha watu dukani kuangalia televisheni.
Alisema kwamba nafasi hiyo waliitumia majambazi hao kujua mwenendo wa fedha, kabla ya kuvamia na kupora.
“Wakati wanavamia majambazi hao, hapakuwa na ulinzi wowote dukani hapo na baada ya kufanikiwa, majambazi waliondoka na gari aina ya Suzuki,” alisema kamanda huyo.
Alieleza kwamba tukio hilo lilitokea masafa mafupi kutoka ofisi za Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Zanzibar, na askari wa FFU wanaolinda tawi hilo walijaribu kusonga mbele kupambana na majambazi hao, lakini hawakufanikiwa.
Habari zaidi zimeeleza kwamba kasi ya askari hao katika kukabiliana na majambazi hao haikwenda sambamba na muda wa tukio, kwa vile walifika majambazi wakiwa wamekwisha kuondoka.
Kamanda huyo alisema kwamba hilo ni tukio la nne la uporaji wa kutumia silaha kutokea katika mkoa huo tangu Januari, mwaka huu.