WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, John Magufuli, anakabiliwa na wakati mgumu kutokana na baadhi ya wanasiasa wenzake kuanza kumpikia majungu, imebainika.
Habari za uhakika kutoka vyanzo mbalimbali, zinaonyesha kuwa kwa muda sasa, Magufuli anaundiwa ‘zengwe’, nia ikiwa ni kufifisha rekodi ya utendaji kazi wake serikalini.
Mashambulizi dhidi ya Magufuli yanaendeshwa na pande kadhaa, ikiwamo Wizara ya Miundombinu ambayo imeundwa kutokana na wizara mbili za Ujenzi, na Mawasiliano na Uchukuzi.
Upande mwingine unaomshambulia waziri huyo, ni ule unaojitahidi kufanya kila liwalo, ili kuhakikisha anawekwa nje ya Baraza la Mawaziri.
Chanzo cha habari kimesema hata kuteuliwa kwake kushika nafasi hiyo, ni kutokana na Rais Jakaya Kikwete kuthamini utendaji kazi wake ambao ulitambuliwa na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.
Kwa muda sasa, imebainika kuwa Wizara ya Miundombinu imekuwa ikijitahidi kukwepa lawama kwa kumsukumia Magufuli udhaifu mwingi unaoikabili wizara hiyo.
Miongoni mwa udhaifu huo ni kushindwa kudhibiti makandarasi wanaojenga barabara mbalimbali ambazo zimechelewa kukamilishwa.
Aidha, kumekuwapo habari kwamba waziri huyo amehusika na upotevu wa fedha kadhaa, lakini wanaotoa tuhuma hizo, wameshindwa kuthibitisha.
“Kinachofanywa sasa ni kujaribu kuonyesha kuwa Magufuli hafai, wanapoulizwa maswali, badala ya kuyajibu, wanafupisha mjadala kwa kumsingizia Magufuli,” kilisema chanzo cha habari.
Mpango unaandaliwa sasa kuhakikisha kuwa baadhi ya mambo mengi yaliyofanywa na Magufuli, ama yanabadilishwa, au yanafutwa.
Miongoni mwa hayo ni mpango wa ujenzi wa nyumba za serikali, na uhamishaji watu waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara.
Kuhusu hifadhi ya barabara, sasa kuna ‘siasa’ inaendeshwa ili kuruhusu watu waliojenga ndani ya maeneo hayo kuendelea kuishi hadi hapo upanuzi utakapofanyika.
Tayari Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Milton Mahanga, ameliambia Bunge kuwa sheria hiyo ya hifadhi inaangaliwa kwa lengo la kuihuisha.
Magufuli jana alizungumza na Tanzania Daima kuhusu ‘zengwe’ linalosukwa dhidi yake, na kusema hata yeye anashangazwa na mambo yanayozushwa dhidi yake.
“Yapo baadhi ya mambo yananishangaza, lakini sina ugomvi na mtu, na wala sitaki mnigombanishe, kinachofanywa sasa ni watu kuzungumza kutokana na uhuru walionao.
“Kama kuna mabaya niliyafanya, wa kuhukumu ni Watanzania, na Mungu pekee, mimi siwezi kusema lolote,” alisema Magufuli nje ya Ukumbi wa Bunge.
Alisema anachofanya sasa ni kujiandaa kutekeleza kwa kasi, nguvu na ari mpya, majukumu aliyopewa na Rais Kikwete katika wizara anayoiongoza sasa.
“Wakati wao wanazungumza, mimi najizatiti kutekeleza Ilani ya chama changu na maelekezo niliyopewa na Mheshimiwa Rais Kikwete, watu wanahoji kuwa mbona niko kimya, ndiyo, niko kimya kwa sababu nilikuwa najifunza ili niijue wizara.
“Muda wa maneno sasa sina, ninachojua ni kazi tu, kama kuna mabaya yanaandaliwa na wabaya wangu, mimi hayo hayanikoseshi usingizi, kwani katika siasa ni mambo ya kawaida,” alisema.