MHANDISI wa Kampuni ya Ujenzi ya M/S Jov, Aaron Kibona (40), amesomewa mashitaka manne, likiwamo la uhujumu kwa kughushi hundi ya dola 890,566.31 za Marekani (zaidi ya sh bilioni moja).
Kibona alisomewa mashitaka jana akiwa kitandani katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambako amelazwa akidaiwa kuugua ini na shinikizo la damu.
Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Mrakibu Mwandamizi, Charles Kenyela, mbele ya Hakimu Catherine Levocate, alidai Kibona, alighushi hundi hiyo kati ya Mei 19 na Septemba 29, mwaka jana mkoani Dar es Salaam.
Kenyela alidai kuwa mshitakiwa akiwa na wenzake, alighushi hundi hiyo akijitambulisha kuwa yeye na wenzake ni watumishi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wakati wakijua si kweli.
Alizitaja hundi zilizoghushiwa kuwa ni zenye namba DNB 71a iliyotolewa Mei 19, 2005 yenye thamani ya dola za kimarekani 289,311.76; na hundi nyingine ilitolewa Septemba 5, 2005 ikiwa na namba DNB 75a za dola 479,791 za Marekani.
Hundi nyingine ilikuwa na namba DNB 92a iliyotolewa Julai 20, mwaka jana ikiwa ya dola 121,463.55 za Marekani.
Alidai kuwa hundi zote zilitumwa kutoka Benki ya EuroAfrica ya Dar es Salaam katika akaunti namba 7058-07-24440 kwenda Benki ya Norske ya Norway.
Kenyela aliyataja mashitaka mengine yanayomkabili Kibona kuwa ni kula njama za kughushi hundi hizo, kughushi hati za malipo kwa kutumia jina la TANROADS na wizi katika Benki ya EuroAfrica.
Mshitakiwa alikana mashitaka yote. Hakimu Levocate alimnyima dhamana baada ya kukubaliana na hoja ya Mwendesha Mashitaka aliyedai kuwa, mshitakiwa ameiba kiasi kikubwa cha fedha. Kesi hiyo itatajwa tena Julai 18.