Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Maajabu ya Mramba
Maajabu ya Mramba
By Habari Tanzania | Published  07/4/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
Na Martha Mtangoo, Dodoma

MBUNGE wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), amemlalamikia Waziri wa Miundombinu, kwa kujitengea sh bilioni 17 kujenga barabara moja ya eneo lake, na kuacha sehemu nyingine nchini zikiwa taabani.

Selelii, alisema Mramba ametenga mabilioni hayo, kujenga barabara ya Marangu-Tarakea yenye urefu wa kilometa tisa.

Alisema kati ya kiasi hicho, sh bilioni 10 ni za ndani, ilhali sh bilioni saba ni za nje.

Selelii alisema Mramba ametenga fedha hizo huku akijua kuwa ujenzi wa barabara hiyo hauko kwenye ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), na ahadi za Rais Jakaya Kikwete.

Alisema barabara hiyo ni ya kuunganisha kata, na kwamba kipaumbele kilipaswa kuwekwa kwenye barabara za kuunganisha mikoa.

Mbunge huyo alisema wakati Mramba akijitengea mabilioni hayo kwa ajili ya barabara ya kuunganisha kata, Barabara ya Nyakanazi-Sumbawanga yenye urefu wa kilometa zaidi ya 400, imetengewa sh milioni 300 tu.

Alisema inashangaza kuona barabara ya Marangu-Tarakea, yenye kilometa tisa inatengewa sh bilioni 17; ilhali mara zote inaelezwa kwamba kilometa moja inaweza kujengwa kwa sh milioni 300. Kwa kilometa tisa, sh bilioni 2.7 zingetosha kuifanya kazi hiyo.

Kwa sababu hiyo, alisema hawezi kuunga mkono hoja ya waziri, na akatoa mwito kwa wabunge wengine kumuunga mkono.

Jana alitangaza kutounga mkono makadirio ya matumizi ya bajeti ya Wizara ya Miundombinu kwa mwaka wa fedha 2006/2007 kutokana na bajeti hiyo kutotenda haki kwa wakazi wa mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa.

 Selelii alisema bajeti hiyo haijatenda haki kwa mikoa ya Magharibi na Kanda ya Ziwa kwa kuwa hakuna fedha zilizotengwa kujenga barabara.

 Alisema wizara hiyo imeshindwa kutengeneza barabara za kibiashara ambazo zinaunganisha mikoa na nchi jirani.

Mbunge huyo alimtaka Mramba aeleze vizuri kuhusu ubinafsishaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) ambao utafanyika Agosti, mwaka huu. 

Alisema inasikitisha kuona waziri anashindwa kuweka bayana suala hilo, hasa kutokana na unyeti wa shirika hilo kwa maendeleo ya taifa.  

Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka serikali ichukue tahadhari dhidi ya kampuni za nje zinazokabidhiwa mashirika na taasisi zinazobinafsishwa.

Akitoa maoni ya kamati yake kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara ya Miundombinu iliyowasilishwa na Mramba bungeni jana, Mohamed Misanga, alisema serikali inapaswa kuwa makini katika ubinafsishaji wa mashirika yaliyobaki.

Kamati imeshauri kupitiwa upya kwa mkataba wa kukodishwa kwa kitengo cha makontena cha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili fedha zinazolipwa serikalini ziweze kulingana na ufanisi wa kitengo hicho.  

Alisema lazima uwepo uwazi na utaratibu shirikishi katika kuingia mikataba ya

ukodishwaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Miundombinu ili kuepusha taifa kupata hasara kama ilivyokuwa kwa TTCL na ATCL.  

Alishauri kuharakishwa kwa mchakato wa kuundwa upya kwa shirika jipya la ndegebaada ya kuvunjwa kwa mkataba wa ATCL na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA).  

Kamati ilishauri zichukuliwe hatua za haraka kuondoa kero ya usafiri na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, kwa kuanzisha usafiri wa treni katikati ya jiji na kujengwa kwa barabara za juu.

Katika bajeti yake, Mramba alisema mwaka huu wa fedha, barabara zenye urefu wa kilometa 28, 800 zitafanyiwa ukarabati kwa gharama ya sh bilioni 90.67. Kati ya hizo, wahisani wanatarajiwa kuchangia sh bilioni 36. 478.

 Kuhusu Daraja la Umoja baina ya nchi za Tanzania na Msumbiji, Serikali ya Tanzania imetenga sh bilioni 3.8. Msumbiji imetenga sh bilioni 4.5.

Kwa mujibu wa Mramba, serikali iko katika hatua za mwisho za kuvunja mkataba baina ya ATCL na SAA.

Alisema ATCL sasa ina ndege mbili tu aina ya Boeng 737; moja imekodiwa.

Wizara ya Miundombinu imeliomba Bunge kuidhinisha sh bilioni 463.881 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizoko chini yake kwa mwaka wa fedha wa 2006/07.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.