Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Mfumo wa vyama vingi ufutwe - CUF
Mfumo wa vyama vingi ufutwe - CUF
By Habari Tanzania | Published  07/3/2006 | Habari za Kitaifa | Unrated
na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imeshauriwa kufuta mfumo wa vyama vingi, kwa madai kwamba Zanzibar haijawa tayari kufuata misingi ya demokrasia, na kwamba haijafuatwa tangu kuanzishwa mfumo huo mwaka 1992.

Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wajumbe wa CUF, wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha kwa mwaka wa fedha 2006/07 katika Kikao cha Baraza la Wawakilishi mjini hapa mwishoni mwa wiki.

Mwakilishi wa Viti Maalum, Mtumwa Kheir Mbarouk (CUF), alisema tangu kuanzishwa mfumo wa vyama vingi visiwani hapa, misingi ya demokrasia imekuwa ikitetereka kila uchaguzi unapofika Zanzibar.

Alisema kwamba, kutokana na mambo yaliyoonekana katika uchaguzi uliopita, kuna haja ya kufutwa vyama vyote vya upinzani na kubakia chama kimoja kama zamani.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Wawi kisiwani Pemba, Soud Yussufu Mgeni (CUF), alisema uchaguzi uliopita ulitawaliwa na uvunjwaji sheria, ikiwamo watu wenye sifa kunyimwa haki ya kujiandikisha na kupiga kura.

Alisema kuna baadhi ya watu walipiga kura zaidi ya tano, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za uchaguzi na misingi ya demokrasia. Alieleza kwamba, pamoja na watu kugundulika kujiandikisha zaidi ya mara moja, SMZ imeshindwa kueleza watu hao wamechukuliwa hatua gani za kisheria.

Mwakilishi huyo alitaka serikali ieleze hatua zilizokwisha chukuliwa dhidi ya watu 2,007 waliobainika wamejiandikisha kinyume cha sheria.

Mgeni aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo Zanzibar, alisema kwamba, hivi karibuni mtu mmoja ambaye alipiga kura 15 kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinashinda, alipoteza fahamu baada ya kutakiwa kutoa sh 40,000 za matibabu, alipompeleka mtoto wake hospitalini.

Naye Mwakilishi wa Jimbo la Mgogoni, Daudi Hassan Daudi (CCM), alisema kwamba, bila CCM, wawakilishi wa CUF wasingekuwapo ndani ya Baraza, kwani CCM ndiyo iliyoruhusu mfumo huo wa vyama vingi na kuwapa fursa kuingia ndani ya Baraza kupitia viti vya Pemba.

 “Tuwe makini katika kuwaongoza wananchi, sisi tunajua CUF mtashinda Pemba, lakini kwa nini kila siku mje kusema uongo?” alihoji mwakilishi huyo.

Alieleza kwamba chama cha CUF hivi sasa kinaeneza sera za kuwatenga watu wa Unguja waliopo katika Kisiwa cha Pemba, ikiwa ni pamoja na kuwanyima ardhi kwa ajili ya shughuli za biashara na makazi.

Mwakilishi huyo alisema kwamba, anao mfano wa mtu aliyerejeshewa fedha zake sh milioni 4, baada ya kuuziwa kiwanja Pemba. Alirejeshewa fedha hizo baada ya kubainika kwamba anatoka Unguja.

Mwakilishi huyo alisema kwamba, kuna watu wanataka kuligawa Baraza la Wawakilishi katika mitazamo ya Uunguja na Upemba, akashauri ukumbi wa Baraza uliopo Pemba ‘ufutwe’.

Alisema kwamba, ni jambo la kushangaza kuona Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lina ukumbi mmoja tu, lakini Zanzibar kuna kumbi mbili, jambo linaloibebesha mzigo mkubwa SMZ.

Naye Mwakilishi wa Wete, Assah Othuman Hamad (CUF), alisema kwamba uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa na kasoro nyingi za kisheria. Alitoa mfano kwa kusema Taasisi ya Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilitoa matokeo kabla ya uchaguzi kufanyika.

Tangu kuwasilishwa bajeti ya wizara hiyo, vikao vya Baraza vimekuwa vikitawaliwa na vijembe vya Uunguja na Upemba, pamoja na misimamo mikali ya wajumbe wa CUF kupinga mafuta ya Zanzibar kuwa suala la Tanzania nzima, wakitaka yabaki kuwa ya Zanzibar.


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Your Favorite Articles
View All Favorites
Articles to Read
You Recently Viewed...
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Barua ya Wazi kwa Rais Jakaya Kikwete
  3. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Marshy Abdu
  4. Linda Garner
  5. Nthelezi Nesaa
  6. Prosper Kwigize
  7. Ramadhan Semtawa
  8. Salehe Mmoro
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.