UTATA umeligubika tukio la kukamatwa kwa mfanyabiashara Lucas Mchomba (71) katika Mji wa Tarakea, Rombo mkoani Kilimanjaro, akihusishwa na mtandao wa ujambazi na kumiliki silaha isivyo halali.
Utata huo unatokana na Mchomba mwenyewe kulalamika na kutoa taarifa kwamba, mtu aliyetoa taarifa kwa polisi juu yake kuwa ana silaha anayoimiliki isivyo halali, alikuwa na chuki binafsi zinazojikita kwenye misingi ya kibiashara.
Baada ya kukamatwa Mchomba, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Venance Tossi, alisema kwamba alikutwa na bastola anayomiliki isivyo halali, na kwamba ilifanana na nyingine anayomiliki kihalali.
Tossi alikaririwa akisema kwamba, ni makosa kwa mtu mmoja kumiliki silaha mbili za aina moja. Lakini, Mchomba anadai kwamba, moja ni ‘toy’ aliyonunulia watoto wake kwa ajili ya kuchezea, ambao kwa sasa wako nje.
Amedai kwamba, kutokana na watoto wake kuwa wakubwa na ambao wapo nje ya Tarakea kwa mosomo, ‘toy’ hiyo imekuwa haitumiki na mtu yeyote zaidi ya kuiweka kwenye kabati.
Bastola (‘toy’) inayodaiwa kukamatwa kwa Mchomba ikimilikiwa isivyo halali ilitajwa na Jeshi la Polisi kuwa ni aina ya DIANA M.O.D inayodaiwa kutengenezwa nchini Ujerumani na haikuwa na namba zozote.
Inadaiwa kuwa, msiri huyo, kwa zaidi ya miaka 10, amekuwa karibu na Mchomba, lakini baadaye walitofautiana naye kibiashara.
Mchomba ni mmoja wa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani hapa, ambaye inaelezwa kwamba, alitofautiana kimsimamo na mtu anayetaka ‘kumbomoa’ Mchomba baada ya mtoto wa mtu huyo kuhusishwa na wizi wa pikipiki.
Inaelezwa zaidi kwamba, namba iliyotumiwa kwenye pikipiki hiyo isivyo halali, ipo kwenye gari dogo aina ya Toyota Corolla inayomikiwa kihalali na mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa kuwa baada ya pikipiki hiyo kukamatwa, kijana huyo alikimbilia kusikojulikana ambapo baba yake huyo alianza kumsaka kwa juhudi za kumnusuru asiingie kwenye mkono wa dola.
Mtu wa kwanza aliyeombwa amsaidie kijana huyo kufutiwa kesi ya wizi ni Mchomba, ambaye inadaiwa alikataa kata kata kusaidia masuala yanayohusu wizi.
Mchomba anatuhumiwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwamba, amekuwa akitumia bunduki hizo kuwakodishia majambazi kwenda kupora na kuua watu.
Mchomba ambaye pia anaendesha kampuni ya upasuaji mbao ya Tarakea Timber Company Ltd. (TATICO), wakati zoezi la kupekua nyumba yake likiendelea hakuwapo, na alijisalimisha kwa Jeshi la Polisi Juni 16, mwaka huu.
RPC Tossi alieleza kwamba, Mchomba alikutwa na risasi 14 za bastola, ambazo polisi inadai hazikuwa na maelezo jinsi zilivyopatikana. Mchomba mwenyewe ameiambia Tanzania Daima kuwa, hawezi kumiliki silaha bila kuwa na risasi.
Hata hivyo, RPC Tossi, akizungumza na Tanzania Daima, alipinga madai hayo kuwa iliyokamatwa ni ‘toy’ na si bunduki halali.