WAWAKILISHI wa Chama cha Wananchi (CUF) visiwani Zanzibar, wamepinga suala la mafuta Zanzibar kuingizwa katika mambo ya Muungano, kama walivyokubaliana Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha.
Hayo wameyaeleza wakati wakichangia bajeti ya ofisi ya Waziri Kiongozi ya mwaka 2006/07 katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mjini hapa.
Mwakilishi wa Jimbo la Tumbe, Ali Mohammed Bakar (CUF), alisema Waziri Kiongozi hakupaswa kubeba jambo zito kama hilo kufikia makubaliano kabla ya kupata baraka za Wazanzibari.
“Si muafaka kubeba mambo nyeti kama hayo na kwenda kuyajadili bila ya kushirikisha wananchi,” alionya.
Alisema kwamba kitendo kilichofanyika ni sawa na mtu mmoja kujitokeza mbele ya watu kuizungumzia familia bila ya familia yenyewe kushirikishwa.
Bakar alisema kwamba Serikali ya Muungano wa Tanzania ina maliasili nyingi, ikiwamo madini kama dhahabu, hivyo si muafaka suala la mafuta ya Zanzibar kuingizwa katika orodha ya mambo ya Muungano.
Naye Mwakilishi wa Viti Maalum, Najma Halfan (CUF), alisema kwamba mafuta lazima yabakie mali ya Zanzibar, kwa vile katika orodha ya mambo ya Muungano liliingizwa kinyemela.
Alisema kwamba hivi sasa kuna watu wajanja wanataka kuchukua mafuta ya Zanzibar, lakini alisema suala hilo litaleta matatizo katika siku za baadaye, na kutoa mfano wa Nigeria wanavyokabiliana katika suala la nishati ya mafuta.
“Mafuta ya Zanzibar ni ya kina Jecha, Pandu, Time. Tuwafikirie watoto wetu, watakuja shika mapanga kudai mafuta yao,” alisema mwakilishi huyo.
Alieleza kwamba, katika suala hilo wajumbe wa CUF na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanapaswa kusahau tofauti zao na kulitetea kwa nguvu zote.
Naye Mwakilishi wa Jimbo la Wawi, Soud Yussuf Mgeni, alisema masuala ya mafuta na gesi mwaka 1964 hayakuwamo katika orodha ya mambo ya Muungano, na badala yake yaliingizwa mwaka 1984 kinyemela.
“Uongozi uliokuwapo Zanzibar wakati huo ulikwenda hadi Dar es Salaam kuonana na Waziri Mkuu, wakasema liondolewe na wakakubaliana, lakini hadi sasa halijaondolewa,” alisema Soud.
Alieleza kwamba, ni bora Serikali ya Muungano ikabakia na dhahabu na almasi, na Wazanzibari wakabakia na mafuta yao, kwa vile ndiyo maliasili inayoweza kuwakomboa kiuchumi.
Katika bajeti ya Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, alisema kwamba, katika kikao chao cha pamoja na Waziri Mkuu Lowassa, wamekubaliana kwamba mafuta, gesi na madini yote yafanywe kuwa masuala ya Muungano.
Alisema kabla ya utaratibu huo, mafuta na gesi peke yake ndiyo yalikuwa masuala ya Muungano na ili kurahisisha utaratibu huo, imependekezwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ifanyiwe marekebisho.
Nahodha alisema kwamba, maazimio katika kikao hicho yamependekeza serikali itafute utaratibu bora utakaotumika katika kugawana mapato, kuzingatia utaratibu unaotumika katika baadhi ya nchi kama vile Canada, Norway na Scotland.
“Mapendekezo haya yatapelekwa kwa viongozi wakuu wa Serikali ya Muungano na ya Zanzibar, ili yapatiwe ufumbuzi muafaka kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili za Muungano,” alisema Nahodha.
Suala la mafuta Zanzibar limegeuka ajenda ya kisiasa, na kujadiliwa na wajumbe wengi wa kambi ya upinzani, licha ya kuwapo muafaka wa kumaliza tatizo hilo uliofikiwa hivi karibuni baina ya Serikali ya Muungano na ya Zanzibar.