Habari Tanzania - http://www.habaritanzania.com
Obama atishiwa maisha
http://www.habaritanzania.com/articles/4292/1/Obama-atishiwa-maisha
By Marshy Abdu
Published on 08/10/2008
 
KAMPENI za kuwania kiti cha urais wa Marekani katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, zimepata sura mpya, baada ya mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo kutishiwa kuuawa.

Obama atishiwa maisha
na Mwandishi Wetu


KAMPENI za kuwania kiti cha urais wa Marekani katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Novemba mwaka huu, zimepata sura mpya, baada ya mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo kutishiwa kuuawa.

Polisi nchini Marekani wamethibitisha kuwa wanamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kutoa vitisho dhidi ya mgombea huyo ambaye anawania kuweka historia katika siasa za Marekani.

Polisi wamemtaja mtu anayeshikiliwa kwa tuhuma hizo kuwa ni Raymond Hunter Geisel (22), ambaye alitishia kumuua mgombea urais wa Marekani kupitia Chama cha Democratic, Barack Obama.

Kukamatwa kwa mtu huyo kumetokea siku chache baada ya kura ya maoni kuonyesha kuwa Obama anaongoza katika kinyang’anyiro hicho, dhidi ya mgombea wa Republican, John MacCain.

Mtu huyo alikamatwa majuzi huko Florida. Kwa mujibu wa taarifa kutoka polisi na mahakamani, mtu huyo alinukuliwa akimweleza mwenzake wakati wa semina kuwa atamuua Obama iwapo atachaguliwa kuwa rais wa Marekani.

Vitisho dhidi ya Obama vimekuja siku chache tu kabla hajatembelea Florida. Polisi walieleza kuwa vitisho hivyo vilitolewa na mtu ambaye ana miliki risasi, bunduki na silaha nyingine.

Hati ya kiapo iliyowasilishwa na makachero katika mahakama ya jimbo hilo, inadai kuwa Raymond Hunter Geisel, mkazi wa Marathon, Florida, alitishia “kumteka, kumpa mateso na kisha kumuua Obama, ambaye ni mgombea urais wa Marekani.”

Katika upekuzi uliofanywa katika gari la Geisel na chumba chake cha hoteli huko Miami, ambako Geisel alikuwa akihudhuria mafunzo, walifanikiwa kupata bunduki, risasi-zikiwa ni pamoja na rifle, taa za tahadhari zinazofanana na za polisi, kifaa cha kujikinga mwili, panga na mabomu mawili ya kutupa kwa mkono.

Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha pia kuwa askari hao walikamata pia vifaa vingine vya kijeshi.

Makachero hao wanadai kuwa rafiki wa Geisel aliwaambia kuwa kati ya Julai 25 na 28, Geisel alitumia lugha ya kutishia akisema: “Iwapo atachaguliwa nitamuua mimi mwenyewe.”

Rafiki huyo, ambaye naye alikuwa akihudhuria mafunzo hayo, alimnukuu Geisel akisema kuwa anamchukia George W. Bush, ambaye ni rais wa sasa wa Marekani, na kuwa alikuwa anataka kumpiga risasi.

Hata hivyo, Ijumaa iliyopita, Obama alifanya kampeni katika maeneo kadhaa ya Florida, siku moja baada ya makachero kumkamata Geisel katika Hoteli ya Holiday Inn Express huko Miami.

Katika mahojiano na makachero hao, Geisel alisema hakumbuki iwapo alitoa vitisho dhidi ya Obama na Rais Bush, lakini aliwaambia kuwa iwapo angetaka kumuua Seneta Obama, angeweza kufanya hivyo kirahisi, kwa kumpiga risasi.

Hata hivyo, alisema kuwa aliyasema hayo kwa utani.

Geisel aliwaambia makachero hao kuwa ana matatizo ya akili, ambayo yanamfanya apoteze kumbukumbu kila mara na wakati fulani aliwahi kulazwa katika kituo cha watu wenye matatizo ya akili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Hati hiyo ya kiapo, iliyosainiwa na kachero Charles R. Adie, inaeleza kuwa Geisel “hakuweza kutoa utetezi wowote” kuhusiana na kwa nini alikuwa na silaha hizo na vitu vingine.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa mtuhumiwa huyo alidai kuwa amekuwa akikusanya baadhi ya vifaa hivyo, na kuwa bunduki alikuwa anaitumia kwa kulenga shabaha wakati wa mafunzo aliyokuwa akihudhuria na kuwa analitumia panga alilokutwa nao kufyeka msitu huko Maine, ambako aliishi kabla ya kuhamia Florida Januari.

Alhamisi, Jaji Stephen T. Brown, alitoa amri ya Geisel kuwekwa mahabusu hadi kesi yake itakaposikilizwa, akimwelezea kuwa ni mtu hatari kwa jamii na ambaye haaminiwi kuwa nje.

Jaji huyo alisema kuwa Geisel anaishi katika boti ya uvuvi, hana ajira, na hana muda mrefu tangu ahamie eneo la Florida.

Anatarajiwa kufikishwa mahakamani tena Agosti 18, mwaka huu. Kama upelelezi utakuwa umekamili ataruhusiwa kujibu shitaka linalomkabili.

Wakili wa Geisel, ambaye ameteuliwa na mahakama, hakutaka kusema lolote kuhusiana na mashitaka hayo yanayomkabili mteja wake.

Iwapo atapatikana na hatia, adhabu ya kosa la kutishia maisha ya mgombea urais au makamu wa rais, ni kifungo cha miaka mitano jela.

Hata timu ya kampeni ya Obama nayo ilikataa kusema chochote kuhusiana na tishio hilo.

Vitisho dhidi ya Obama vilianza kuonekana tangu Mei mwaka huu, kiasi cha serikali kuamua kutoa maofisa usalama kwa ajili ya kumlinda.

Aliyekuwa anachuana naye katika kinyang’anyiro hicho ndani ya chama chake, Hillary Clinton, naye tayari alikuwa ameshapatiwa maofisa usalama wa kumlinda, kwa kuwa aliwahi kuwa mke wa rais, lakini John Kerry, mgombea urais wa Democratic mwaka 2004, hakupatiwa mtu wa kumlinda hadi aliposhinda kura za uteuzi.

Maofisa usalama wanaomlinda Obama wameonekana kuwa na wasiwasi tangu wakati huo, na wakati fulani walionekana kuwa na machale wakati mtu mmoja huko Iowa alipopiga kelele akiita “Obama, Obama” na kumkimbilia seneta huyo katika veranda, mara baada ya kumaliza kuhutubia.

Jesse Jackson, naye aliwahi kupewa ulinzi wa maofisa usalama wakati alipokuwa akigombea urais wa Marekani mwaka 1988, baada ya kutolewa vitisho vya kuuawa, wakati Colin Powell, anadaiwa kukataa kugombea urais akihofia kuuawa kwa mkewe, Alma.

Wapiga kura kadhaa wameshasema kuwa hawatampigia kura Obama, kwa sababu wana hofu kuwa iwapo watamchagua anaweza kuuawa na mtu huyo aliyetoa vitisho.