Kitaifa
   Siasa
   Jamii
   Uchumi
   Makala

 

Search


Advanced Search

 »  Home  »  Habari za Kitaifa  »  Kama Zanzibar si nchi, Tanganyika ilijiunga na wilaya?
Kama Zanzibar si nchi, Tanganyika ilijiunga na wilaya?
By Marshy Abdu | Published  08/10/2008 | Habari za Kitaifa | Rating:
Kama Zanzibar si nchi, Tanganyika ilijiunga na wilaya?
Prudence Karugendo


BABA wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikuwa mtu mwenye kanuni ya kujikosoa. Nadhani ni kanuni hiyo iliyomfanya afe akiwa kipenzi cha wote wakiwamo hata wale ambao kwa namna moja au nyingine walibanwa na wadhifa wake.

Alikuwa akiyakiri makosa aliyoyafanya maishani mwake kama binadamu, lakini bila kukosa kuyatolea mambo yaliyosababisha kutokea kwake, sababu ambazo mara nyingi zilimlinda kwa kuonyesha kwamba hakufanya makosa husika kwa kuinufaisha nafsi yake, bali katika kujaribu kuinusuru jamii yake kulingana na hali iliyochochewa na wakati uliokuwapo.

Mara nyingi Mwalimu alikuwa anasisiza kwamba kinapoangaliwa kitu au maamuzi ni lazima kipimwe kulingana na wakati uliopo, akisema kwamba maamuzi kama ya miaka 30 au zaidi iliyopita si lazima yaendelee kuwa sahihi baada ya muda wote huo, si lazima yaendelee kusimama na uthabiti leule wakati dunia ikibadilika.

Alikuwa akitukumbusha kwamba tunapoongelea maamuzi ya wakati uliopita tusisahau kuongelea sababu nzuri za wakati ule za maamuzi husika tukizilinganisha na sababu nzuri za kuendelea kuyaenzi maamuzi hayo kwa wakati tulio nao.

Mfano mwaka 1992 alipoongelea suala la vyama vingi vya siasa, alisema kwamba nchi ilipoamua kufuata utaratibu wa chama kimoja cha siasa ilikuwa na sababu nzuri za kufanya vile kwa wakati ule, ambazo si lazima kwamba zingeendelea kuwa kuwa nzuri kwa mwaka 1992.

Kwa hiyo, akasema kwamba kuongelea vyama vingi haikuwa dhambi kwa mwaka huo, akisisitiza kwamba zilizopaswa kutizamwa ni sababu nzuri za kurudisha au kutorudisha mfumo wa vyama vingi vya siasa za mwaka 1992 na wala si zile zilizosababisha nchi kufuata utaratibu wa chama kimoja, alizoziona kuwa zilikuwa zimepitwa na wakati japo yeye ndiye aliyekuwa muasisi wa utaratibu ule hapa nchini.

Kwa sasa hivi kuna kitu kinachoonekana kama malumbano yanayoelekea kuuchokonoa uhai wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, malumbano ya Zanzibar ni nchi au la.

Tukumbuke huu ni Muungano uliofanywa haraka haraka kwa utashi wa viongozi wakuu peke yao (kwa niaba ya wananchi?), bila wananchi kupewa fursa ya kuujadili mustakabali wa nchi zao kwa kina - Tanganyika na Zanzibar.

Bila shaka zilikuwapo sababu nzuri za kufanyika kwa uharaka huo kwa wakati ule mwaka 1964, sababu ambazo sina uhakika kama bado ziko vilevile hata baada ya miaka 44 ya uhai wa Muungano. Kwa sasa tunachohitaji kukiangalia ni sababu nzuri za mwaka 2008 za kuutazama upya muundo wa Muungano wetu.

Inaelezwa kwamba moja ya makubaliano ya Muungano huu ni kwamba Zanzibar ingebaki ni nchi ndani ya Muungano, ikiwa na rais wake (executive president), Baraza lake la Mawaziri, Bunge na Mahakama kama tunavyoiona kwa sasa.

Sababu zinazotolewa juu ya makubaliano hayo ni kwamba hiyo ilikuwa ni kuiepusha Zanzibar isije ikamezwa na Tanganyika. Sasa anayekataa kuwa Zanzibar si nchi haoni kuwa anataka kuifanyia mchezo wa ‘kanyaboya’ Zanzibar?

Muda wote Wazanzibari wanaamini kuwa makubaliano ya Muungano ni wao kubaki na nchi yao na Serikali yao ya Mapinduzi ndani ya Muungano. Leo hii kuwaambia Zanzibar si nchi si ni sawa na kuwapiga changa la macho.

Hivi kweli tunaamini kwamba wanaweza kubaki kimya wakikubali kuwa muda wote wamekuwa wakibebeshwa mdoli mgongoni na si mtoto halisi?

Watanganyika ndio tuliokubali kuipoteza Tanganyika yetu ndani ya Muungano kwa imani kwamba kutokana na ukubwa wake, isingeweza kumezwa na kusahaulika.

Hatukujiuliza ilikuwaje dola ya Kirumi iliyokuwa imeenea karibu nusu ya dunia ikaweza kumezwa na kubaki tu kwenye makabrasha ya historia. Ila nina uhakika hoja hiyo ingeletwa kwa Mwalimu wakati huu angeitolea maelezo yaliyo tofauti na yale aliyoyatoa mwaka 1964.

Hata hivyo, Wazanzibari wanaliona suala la Tanganyika kukubali kujitoa kafara, ili kuupisha Muungano kama mchezo wa kisanii kwa vile wanaamini kuwa kilichofanyika ni Tanganyika kujibadilisha jina tu.

Wanahoji kwamba kuna ushahidi gani unaoonyesha kwamba Tanganyika ilikufa na kuzaliwa taifa jipya la Tanzania? Wanadai kwamba kilichoonekana kimekufa na kubaki jina tu ni Zanzibar ambayo ilipoteza nafasi zake zote katika ushirikiano wa kimataifa, kama vile kiti chake kwenye Umoja wa Mataifa na OAU, wakati vile vilivyokuwa vinakaliwa na Tanganyika ndivyo vilivyogeuka na kukaliwa na Tanzania.

Hoja ni kwamba vyote vilipaswa kufutwa kutoa nafasi kwa taifa jipya la Tanzania kuomba uanachama upya kitu ambacho hakikufanyika.

Ndiyo maana Wazanzibari hawataki kuambiwa kwamba Zanzibar si nchi, madai ambayo ukiyatazama kwa kufuata haki, yana ukweli wake. Maana kinachoonekana hapa ni kwamba Zanzibar ilichomekwa ndani ya Tanganyika iliyogeuka kuwa Tanzania kwa mawazo yale yale yanayojionyesha kwa sasa kwamba visiwa vile vilipaswa kuwa sehemu ya Tanganyika.

Kauli hizi za Zanzibar si nchi zinaelekea kuyashadidia mawazo ya aina hii ambayo ni lazima yalete hisia za kwamba basi Muungano ni kiini macho.

Na hii inawafanya Watanganyika waonekane walikuwa na dhana hii tangu awali ya kutoikubali hadhi ya Zanzibar kama nchi, kitu kinachoweza kuchukuliwa kuwa ndicho kilichoshinikiza kuharakisha kuiweka Zanzibar pamoja na Tanganyika, ili ihesabike kama sehemu ya Tanganyika ikiwa imefunikwa na kitambaa cha Muungano.

Wazanzibari wazalendo wanayo haki ya kushtuka wanapoambiwa kuwa nchi yao si nchi. Tujikumbushe Tanzania tulivyolazimika kupigana vita mwaka 1978 baada ya Idi Amin wa Uganda kuvamia sehemu ndogo ya ardhi ya Tanzania, kaskazini mwa Mkoa wa Kagera. Je, mtu yule angesema Tanzania si nchi hali ingekuwaje? Inabidi tujiepushe na dhana ya mkuki kwa nguruwe.

Imejitokeza misamiati mbalimbali katika kuilegeza hoja hii ikionyesha kuwa kilichomaanishwa ndicho kisichoeleweka vizuri. Kuna wanaosema kwamba kilichomaanishwa ni dola wakati wengine wakisema jamhuri na kadhalika. Lakini, chanzo cha yote ni tamko la kwamba Zanzibar si nchi.

Na sidhani kama aliyetamka hivyo hiyo misamiati alikuwa haijui. Vyovyote iwavyo, Wazanzibari walipopashikilia, ambako na mimi napaunga mkono, ni pale wanapouliza kwamba kama Zanzibar si nchi huu Muungano wa Tanzania ni wa nchi na wilaya?

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hakukosea kusema kwamba Zanzibar si nchi, kwa dhamana aliyo nayo ni lazima asimamie katiba ya nchi inavyotamka. Lakini pia wananchi wazalendo wa Zanzibar wanaolaani tamko la Pinda, nao vilevile hawajakosea maana wanasimamia haki yao ya msingi ya kuienzi nchi yao wanayoona inadhalilishwa na tamko la Pinda.

La msingi ni kuupima usahihi uko wapi kati ya anayesimamia utaratibu uliowekwa na wanadamu na anayesimamia haki iliyowekwa na Mwenyezi Mungu.

Wapo wanaoyaona madai haya kama upuuzi wakisema kwamba mbona Watanganyika nao hawadai nchi yao? Wenye mawazo ya aina hii ni wazi kwamba kuna kitu kinawakwepa. Ni kwamba kutojali kwa Watanganyika, hakutokani na kutoipenda nchi yao.

Ikumbukwe kwamba baada ya Muungano hakuna kitu ambacho Watanganyika walipoteza zaidi ya jina tu la nchi yao ambalo ni jambo la kawaida. Amiri Jeshi Mkuu wao walibaki naye, jeshi lao walibaki nalo, mahusiano ya kimataifa walibaki nayo, kiti chao katika Umoja wa Taifa walibaki nacho, Hazina na Benki Kuu pamoja na sarafu vilibaki vilevile, na kadhalika. Sasa kelele wapige za nini?

Wanaozibeza hoja za Wazanzibari wanaegemea zaidi kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano. Ila inapaswa izingatiwe kwamba katiba ni utaratibu unaotengenezwa na wanadamu. Siamini kama hiyo ni sababu tosha ya kumfanya mtu akae kimya hata pale anapoona haki yake inaminywa.

Tuchukulie mfano wa wazalendo wa Afrika Kusini. Wakati wanaanza harakati za kudai haki nchini mwao, tayari nchi ile ilikuwa na katiba iliyokuwa ikihalalisha yale waliyokuwa wakiyapinga.

Kwa nini wazalendo wale waliungwa mkono na jumuiya ya kimataifa, Tanzania ikiwa mstari wa mbele, kama katiba ni mwanzo na mwisho wa kila kitu katika nchi husika? Hapa inabidi tuelewe kuwa ipo haja ya kudai haki ikibidi pale katiba inapoonekana kuiminya haki hiyo.

Harakati zote za kudai haki husababishwa na taratibu halali, ambazo tunaweza kuziita katiba, zinazokuwa zimetengenezwa kwa namna ya kupindishwa, ili zipendelee upande mmoja sawia na kuupunja upande mwingine.

Kwa hiyo, haitoshi kubaki tukijiaminisha kwamba madhali katiba ya Jamhuri ya Muungano ipo, haipaswi kuangaliwa wala kufikiriwa kitu kingine kinachohusu Muungano wetu nje ya kilichomo kwenye katiba hiyo. Tukiilazimisha hali hiyo tutakuwa tunachochea kuanzishwa kwa harakati za kuuvunja Muungano.

Ninajiuliza pia iwapo Muungano upo kwa manufaa ya nani? Maana wakati mwingine huwa nashawishika kuamini kuwa upo kwa manufaa ya viongozi tu, kutokana na juhudi wanazozionyesha za kuulinda na namna zilivyokaa. Sababu kama Muungano upo kwa manufaa ya Watanganyika na Wazanzibari ambao ni wananchi wa nchi hizi mbili, marehemu Tanganyika na Zanzibar, kwa nini wananchi hawa wasiachwe wakayaona hayo manufaa na kisha wao wakauona umuhimu wa kuulinda muungano kwa gharama nafuu, kuliko ilivyo sasa ambako kodi zao zinakamuliwa katika kiwango cha kutisha kuulinda huo muungano tena wao wakinyooshewa vidole na vitisho kedekede kana kwamba ndio maadui wa muungano huo?

Maoni yangu ni kwamba; ili tuulinde na kuuendeleza huu Muungano wetu, inabidi tuutizame bila woga wala hofu tukiamini kuwa ni wetu uliopo kwa manufaa yetu, muungano wa nchi mbili.

Baada ya hapo tuziangalie dosari ambazo ama ziliachwa makusudi kwa sababu nzuri za wakati ule au hazikujionyesha kulingana na wakati uliokuwapo, na kisha tuzishughulikie kulingana na wakati wa sasa. Namaanisha kwamba tuuangalie Muungano wetu tukizingatia sababu nzuri za kuwa nao kwa sasa tukiziacha zile za mwaka 1964.

Hila zozote za kutaka kuuficha ukweli huo zitauangamiza Muungano, na wale wanaosema kwamba hawataki uwafie mikononi mwao watakuwa wa kwanza kulibeba jeneza la Muungano. Na tusipokubali kwa hiari tutashtukia tunalazimika kuukubali ukweli wa kwamba Zanzibar ni nchi pamoja na udogo wake.

prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 5120


How would you rate the quality of this article?
1 2 3 4 5
Poor Excellent
Add comment
Comments


Article Options
Popular Articles
  1. Unaifahamu Jambo Forums?
  2. Ghorofa Jijini lanusurika kuungua moto
  3. Britsh M.P. calls for the suspension of aid to Tanzania.
  4. Is Tanzania a safe place to invest?
  5. Nitaendelea kugombea nafasi za kisiasa- Balozi Karume
No popular articles found.
Popular Authors
  1. Habari Tanzania
  2. Mzee Mwanakijiji
  3. Nthelezi Nesaa
  4. Linda Garner
  5. Marshy Abdu
  6. Prosper Kwigize
  7. Salehe Mmoro
  8. Ramadhan Semtawa
  9. Manyerere Jackton
  10. Ndesanjo Macha
No popular authors found.