Ukali wa mchuano huo sasa umesababisha Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe na mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho anayepewa nafasi kubwa ya kushinda, Victor Kimesera, waanze kutumia helikopta kuwavuta wapiga kura zaidi ya 70,000 wanaotarajiwa kujitokeza kwa wingi keshokutwa Jumapili kuchagua mbunge wao.
Wakati CHADEMA wakitumia helikopta, CCM kwa upande wake imepeleka makada wake kadhaa maarufu wanaoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa, Katibu Mkuu wao, Yussuf Makamba na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, wanaopiga kampeni wakisaidiwa na kundi la burudani la Tanzania One Theatre linaloongozwa na Kapteni John Komba.
Tukio la kutua kwa helikopta ya CHADEMA katika kampeni hiyo katika siku yake ya kwanza jana, kulisababisha kuibuka kwa mvutano mkubwa kati ya vyama hivyo viwili, hali iliyosababisha Jeshi la Polisi kuingilia kati.
Katika tukio moja, Jeshi la Polisi jana lililazimika kumteremsha kutoka jukwaani Kapteni Komba na kundi lake la TOT, baada ya kada huyo wa CCM ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho tawala kuvamia eneo la kampeni lililokuwa likitumiwa na mgombea ubunge wa CHADEMA aliyekuwa akisindikizwa na viongozi takriban wote wa juu wa chama hicho.
Kushushwa kwa Komba kutoka jukwaani kulikuja baada ya CHADEMA kulalamikia kitendo cha kundi hilo kuvamia eneo la Kijungu ulipokuwa ukifanyika mkutano wa kampeni wa chama hicho , huku likijua kuwa ratiba ilikuwa ikionyesha kwamba, chama hicho cha upinzani ndicho kilichokuwa kikitakiwa kuendesha kampeni zake katika eneo hilo.
Mara baada ya TOT kuzuiwa, Mbowe aliyehutubia kwa mara ya kwanza katika kampeni hizo jana, huku akiwa ameongozana na Katibu MKuu wake, Dk. Willibrod Slaa, na mgombea ubunge Kimesera, aliwaeleza mamia ya wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kwamba, CHADEMA ilikuwa ikitarajia kuwa uchaguzi utakuwa huru na wa haki.
Aliwataka wananchi kutumia uhuru wao wa kidemokrasia kumchagua mgombea wa CHADEMA na akawataka wasimamizi kuendesha zoezi la kura kidemokrasia, kwani chama hicho kilikuwa hakitaki kuona damu ya wananchi wasio na hatia ikimwagika au Kiteto ikigeuka uwanja wa vita baada ya uchaguzi kumalizika.
Awali kabla ya Mbowe kutua na helikopta Kiteto majira ya saa 7:00 mchana, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu na Kapteni Komba, walikuwa wakiwaeleza wananchi kuwa harakati za CHADEMA kuileta helikopta zilikuwa zimegonga mwamba.
Komba alisikika akiwaeleza wananchi hao kuwa taarifa walizokuwa nazo zilikuwa zikieleza kuwa helikopta hiyo ilikuwa imeharibika huko Nairobi na hivyo isingeweza kwenda katika kampeni kama ilivyokuwa ikitangazwa na viongozi wa CHADEMA.
Kwa upande wake Shekifu, alisema akiwa mkuu wa mkoa alikuwa hana taarifa zozote za kuwasili kwa helikopta na kwamba alikuwa akijua kuwa isingeweza kufika huko Kiteto pasipo yeye kujua.
Hata hivyo ilipofika majira ya saa 7:30, Mbowe alitua Kiteto akiwa na helikopta na kusababisha mamia ya wapiga kura kushikwa butwaa, wakishindwa kujua sababu za makada wa CCM kutangaza kwamba kulikuwa hakuna kitu kama hicho.
Katika hatua nyingine, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jana ilitangaza kuiruhusu CHADEMA kutumia mawakala wake wanaotoka katika maeneo mbalimbali nchini kinyume cha ilivyokuwa imeamriwa na msimamizi wa uchaguzi wa Kiteto.
Katika maamuzi yaliyotolewa na NEC na kufikishwa kwa chama hicho kwa barua ya Februari 20 mwaka huu (juzi), NEC imeipa CHADEMA na vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo kuchagua mawakala wanaowapenda na si lazima wanaotoka katika kata husika.
Barua hiyo yenye kumbukumbu namba EA.75/162/08 kutoka kwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Rajab Kiravu, inafafanua kuwa kifungu cha 57 cha Sheria ya Uchaguzi Namba 1 ya mwaka 1985, kinaruhusu kila chama cha siasa, kwa makubaliano na mgombea, kuweka wakala wa kusimamia upigaji kura katika kituo.
“Sheria ya uchaguzi namba 1 haijaeleza bayana mawakala watoke ndani au nje ya kata/jimbo la uchaguzi,” alisema Kiravu katika barua yake hiyo ambayo inafafanua kuwa, ili jukumu la kuwatambua wapiga kura lifanikiwe, NEC ilitoa maelekezo kwamba ni vema mawakala watoke katika kata anayoishi.
“Hata hivyo, kwa sababu mbalimbali imeonekana kuwa mawakala kutoka katika kata husika wanaweza wasitimize lengo la kuwakilisha na kulinda masilahi ya wagombea husika ipasavyo…kwa kutambua hilo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kikao chake kilichofanyika tarehe 20 Februari 2008, imetoa idhini kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa Bunge katika Jimbo la Kiteto kuweka mawakala wanaowaona wanafaa kulinda masilahi ya wagombea wao hata kama mawakala hao wanatoka nje ya jimbo au kata,” anasema Kiravu katika barua hiyo ya kurasa mbili.
Hata hivyo, Kiravu anaonya kuwa katika kituo cha kupigia kura, mkuu wa kituo ndiye ana madaraka ya mwisho ya kutoa uamuzi katika suala lolote linalojitokeza katika kituo husika.
Alisema kuwa, iwapo mtu hataridhika na maamuzi au jambo lolote litakalotokea katika kituo, anachotakiwa kufanya ni kufuata sheria na kujaza fomu husika.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kuwa chama hicho hakikuridhishwa na uamuzi wa kuwakatalia kuwatumia mawakala ambao wao wanawaona kuwa ndio wanaofaa.
Mbowe aliilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kwenda kinyume cha sheria kuhusu suala la mawakala wa uchaguzi.
“Kila chama kina haki ya kuchagua wakala wake…hawa wenzetu wanakusudia kuiba kura, wanatunyima uhuru wa kuchagua mawakala. Sisi tutaka madiwani na wabunge ndio wawe mawakala wetu,” alisema.
Kutokana na malalamiko hayo, Mbowe akiwa ameongozana na Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, walikwenda kuonana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC na wakamtaka afuate sheria kuhusu suala la mawakala wa uchaguzi na kutotaka kusikia matakwa ya chama fulani.
“Viongozi tutakuwa mawakala, tutalinda kura zetu. Tuko tayari kuumia katika uwanja wa mapambano. Tumeiomba NEC isimamie haki na wasiwe wanasiasa,” alisisitiza Mbowe wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi.
Kwa upande mwingine, Kiravu alisema katika barua yake kuwa, sheria ya uchaguzi inamtaka kila wakala kula kiapo cha kutunza siri mbele ya msimamizi wa uchaguzi au msaidizi wake, kabla ya kwenda kusimamia uchaguzi katika kituo.
Hata hivyo, alisema kuwa pamoja na msimamo wa sheria, ambayo haijaeleza kipindi mahususi cha kuwaapisha mawakala, tume imeona ni vema kuweka ukomo wa siku ya kuwaapisha mawakala ili kutoa nafasi kwa msimamizi wa uchaguzi na wasaidizi wake kutekeleza majukumu mengine.
Alisema kuwa tume imeamua kuwa leo (Ijumaa) ndiyo itakuwa siku ya mwisho kwa kuwaapisha mawakala ili kuwawezesha na mawakala hao kusambaa katika vituo vya kupiga kura kabla ya siku ya uchaguzi huo, keshokutwa Jumapili.
Wakati huo huo, NEC imelaani vurugu zilizotokea siku kadhaa jimboni humo katika mikutano ya kampeni na kusababisha kujeruhiwa kwa viongozi wa CHADEMA.
Taarifa ya NEC iliyosainiwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Lewis Makame, ilieleza kuwa, tume hiyo imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za vurugu ambazo zimetokea katika jimbo hilo wakati wa maandalizi ya uchaguzi mdogo.
“Tume inachukua nafasi hii kukemea vitendo vyovyote ambavyo vinafanyika kwa lengo la kuathiri, kuvuruga au kuchafua mchakato wa uchaguzi mdogo huo,” alisema Makame.
Makame alichukua fursa hiyo kuwakumbusha wadau wote katika uchaguzi huo kuzingatia sheria, maelekezo ya Tume na maadili ya uchaguzi wakati huu wa kampeni na siku ya kupiga kura.
Kwa upande mwingine, Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, naye amelaani vurugu hizo na kuviasa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi huo kuheshimu kanuni za maadili ya vyama hivyo ili kuepuka vurugu, ubabe na uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema wajibu wa vyama vya siasa ni kufanya siasa za kistaarabu, kuheshimu sheria za nchi, kudumisha amani na utulivu wakati wote na sehemu zote watakapofanya shughuli za kisiasa hasa katika kampeni za uchaguzi.
Hata hivyo, Tendwa alisema kuwa hajapata taarifa rasmi kutoka kwa CHADEMA kuelezea kushambuliwa na kuumizwa kwa viongozi wake kwani yeye amezisoma katika vyombo vya habari.
Tendwa alitoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kutimiza wajibu wake chini ya sheria za vyama vya saisa namba 1(b), ambayo inalitaka Jeshi la Polisi kulinda mikutano ya vyama vya siasa ili kuepuka vitendo vya uvunjaji wa amani.
Alisema kuwa hiki si kipindi cha malumbano bali ni kipindi cha kutekeleza wajibu kwa mujibu wa sheria na kulitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wote waliohusika na vurugu hizo na kuwafikisha katika vyombo vya sheria bila kujali itikadi zao za kisiasa.