MWANANGU mtabisha nikiwaambia kastama kea kwenu ni ziro? Mbona siku zote tulifunzwa kwamba mteja ni mfalme wajameni? Kumbe kauli hii ya mteja ni mfalme haiwahusu Wabongo sio? Kama sivyo mbona hatuoni ubora wa huduma kwa wateja katika nyanja zote? Nawaapia tangu siasa, michezo, jamiii na eneo lolote utakalo, hakuna kabisa hicho kinachoitwa kwa kimombo customer care! Huko simo mwanakwetu.
Kwani si mmeshuhudia bosi wa Benki Kuu alivyofutwa kazi? Kwani mwadhani kikubwa ni kipi mwanakwetu? Angekuwa anajua kwamba Watanzania wote ni wateja wake si angelikuwa anawahudumia kama mfalme?
Mwanakwetu wambea wanateta eti alijikita kuhudumia makampuni ishirini na kitu hivi yakajichotea zaidi ya bilioni mia moja! Astagharafulilah walhai! Eti mipesa yote hiyo ikaenda kwenye matumbo ya watu bila uhalali wowote? Nasikia kuna walioghushi hadi nyaraka ili washiriki ulaji bila kunawa. Hii ni soo washirika. Wacha tu nijitoe kabla sijamwagiwa tindikali. Huko simo miye.
Hayo ya Daudi na mapesa ya dhuluma tuachie kikosi kilichoundwa kufuatilia. Turudi kwenye ya kwetu. Si nimewaambia hapa Bongo wanasema mteja ni mfalme, lakini hakuna anayetekeleza kwa vitendo? Kwani kwenye siasa, wateja si ni wapiga kura?
Mbona waliochaguliwa walipaswa watuhudumie kama wafalme sisi tuliowachagua? Kwani bado ni siri kwamba baada ya kura wakubwa wakishapata kula wengi wanasahahu walitupigia magoti na kutuamkia shikamoo wakati wa kuomba kura?
Kumbe ukishapata kura na kula ule ufalme wetu unafanya “abauti tan” na kugeuka utumwa? Hamjayashuhudia haya Yarabi? Fuatilia kauli za uliyemchagua wakati wa kuomba kura kisha linganisha na matendo yake baada ya kupata kula. Huko nishawaambia simo maana hawakawii kunikubenea! Simo huko kabisaaa!
Huko kwenye maofisi yanayopaswa kutoa huduma mbona ndiko hakuna cha ufalme hata ule wa kufikirika? Hili tuliseme taratibu, huko kwenye maofisi ya serikali mbona karibu yote ukienda kupata huduma unaonekana kama uchafu usiostahili? Ina maana nyie hamjakutana na zile kauli za “njoo kesho….” Au “jaribu tena neksti wiki”?
Ndiyo ufalme wa mteja huo? Mbona kuna afisi unaenda unakutana na wahudumu wa ofisi hiyo wakinywa uji badala ya kutoa huduma? Ina maana ulishindwa kujidamkia mapema unywe uji huko nyumbani kwako hadi ubebane nao ukanywee kwenye ofisi za umma? Eti mwataka turudishe wanyapara sio? Mbona unalipwa mshahara hata kama ni kiduchu halafu unaleta za kuleta? Huko nishasema lazima nijitoe.
Nasikia kuna hospitali mgonjwa akipelekwa manesi wanamtazama kama kero au kitimoto kilichokatiza masjid! Kama uuguzi unawashinda si muende Gezaulole mkajilimie nafaka? Mwang’ang’ania kazi za wito ilhali hamna wito?
Mmefikia huko kwenye kuingilia fani za watu? Muuguzi aliyefunzwa akafunzika anaweza kuendelea kujiremba hospitalini badala ya kuhangaika kusafisha vidonda vya wagonjwa na kuwafariji wale wanaogugumia maumivu? Kwani kwa muuguzi mteja si ni mgonjwa? Hata kama hawaombi watu waugue, lakini ukweli si ni kwamba kula yao inategemea maradhi? Huko nishawaambia lazima nichomoke wasije wakakataa kunipa panadol siku nikienda kutafuta huduma. Simo tena simo kabisaaaa!
Kwani wale maofisa ambao wanaenda ofisini kusaini kitabu cha mahudhurio kisha wanaondoka nao wako kundi gani? Walipwa mshahara kisha twaja ofisini twakuta umetundika koti kisha ukatokomea unakokujua?
Ndio kastama kea hiyo? Msusuru wa watu unajipanga ofisini kwako tunaishia kuambiwa eti umeenda lunch? Uliajiriwa ili uende lunch saa nne urudi saa nane? Kwani hayo ni siri mwanakwetu? Mimi nshawaambia tena huko lazima nijichomoe kabla hajanizaba makofi ya kelbu.
Kwani mwadhani hayo ya kutokumjali mteja yako kwenye ofisi za umma peke yake? Nakuapia zipo hata baadhi ya ofisi binafsi kuingia huko ni kero sawa na kuingia jehanam! Ninyi hajawahi kukutana na masekretari ambao wameamua kumiliki ofisi kuliko wamiliki wenyewe?
Ukiwaeleza shida wanabenua midomo kama vile umewatusi? Ambaye hajawahi kukutana na watu wa aina hiyo anibip mimi nitampigia kumtajia kwa majina hao watu wasiofundwa namna ya kumhudumia mteja. Mbona waswahili walishasema siku nyingi kwamba biashara haigombi?
Matatizo yako na mumeo au mkeo wayapeleka kwa wateja? Ustaarabu mbona hauuzwi wajameni? Mbona wakati mwingine hata kituo cha polisi wapata mapokezi mazuri kuliko kwenye biashara zenu tunazowaletea pesa. Nikimbie huko kukingali mapema mtoto wa mama miye.
Hivi Wabongo lini watajifunza kutoa huduma jamani? Nawaambia hata huko kwenye mabaa na migahawa, wenyewe mnaita hoteli huduma ni duni mwanakwetu. Kwani mara ngapi mteja anaingia na kukaa zaidi ya nusu saa bila kuulizwa haja yake ni ipi?
Mwadhani watu wanakuwa wameenda kuuza sura wanapokuja sehemu za huduma? Eti na maeneo kama hayo kuna mtu anaitwa meneja? Eti na mshahara analipwa, lakini kazi haziendi? Nawaambia Wabongo mkizubaa ajira zenu zitachukuliwa na jirani zenu hao watoto wa Kibaki, ninyi mbaki mkiduwaa. Huko simo.
Mwadhani kama kweli mngejua mteja ni mfalme na mkafanya hivyo haya mambo ya hongo, rushwa na takrima yangekuwepo? Kwani ninyi hamjawahi kukumbwa na haya makasheshe ya kuambiwa eti faili halionekani? Mbona nasikia ukiwawezesha wahusika jalada linaonekana kwa kasi ya mwanga? Hiyo ndiyo customer care siyo? Au ndio mwaleta ule uhuni kwamba kila mtu anakula mezani kwake?
Nawaapia tutaunda tume iwasake wote mlioshindwa kuhudumia wateja kama wafalme halafu tuwaonyeshe cha mtemakuni. Huko simo mwanakwetu. Najitoa katika hayo yote, tena simo kabisaaaa!
kevinmakyao@hotmail.com
0784 265072